Na Joyce Kasiki,Timesmajira Online,Dodoma
MAKAMU wa Rais Dkt.Philip Mpango amezindua maadhimisho ya wiki ya sheria nchini huku akionyeshwa kukerwa na vitendo vya rushwa kwa Mahakimu na Majaji na Mawakili.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa maadhimsho ya wiki ya sheria nchini Dkt.Mpango amesema katika nyakati tofauti amekuwa akipokea malalamiko kutoka kwa wananchi kuhusu muhimili wa Mahakama na vyombo vingine kama polisi na Magereza.
Dkt.Mpango amesema baadhi ya malalamiko hayo ni pamoja na baadhi ya mahakimu,mawakili na majaji kutokuwa waaminifu kwa kudai rushwa kinyume cha viapo vyao .
“Mfano,kuna minada ya mifugo ambayo inakamatwa kwenye maeneo ya hifadhi mara kadhaa,mfano Mbeya kule tumeletewa malalamiko, minada hiyo inazuiliwa kwa amri ya mahakama tena wakati mwingine unashituka kabisa hiyo mahakama imekaa jumapili ,au faini zinazoamriwa ni ndogo mno kwa hiyo mwenye mifugo yake analipa faini baada ya nusu saa anarudisha mifugo kwenye hifadhi ,
“Lakini pia nimepokea malalamiko ya fedha za kigeni ambazo zinakamatwa mipakani zinapotea mikononi mwa mahakama lakini pia wananchi wanalalamikia kwamba hukumu zinapindishwa ili kumpa ushindi mwenye fedha pamoja na gharama kubwa za uendeshaji wa kesi na kulipa gharama za mawakili .”amesema Dkt.Mpango
Vile vile amesema,wananchi wanalalamikia hukumu kuandikwa kwa lugha ya kingereza lakini pia watuhumiwa wanakaa mahabusu muda mrefu wanasubiri uchunguzi kukamilika huku wananchi wengine hawana elimu ya sheria.
Pia Dkt.Mpango amesema,malalamiko mengine anayoyapokea kutoka kwa wananchi ni baadhi ya maeneo kutokuwa na mahakama hivyo hutembea umbali mrefu kutoka walipo wananchi mpaka mahakamani .
“Aidha wananchi wanalalamikia mila na desturi potofu zinazokinzana na sheria na hasa kuhusu mirathi na umiliki wa ardhi kwa wanawake na haki za watoto,mimi naamini changamoto hizi zinaepukika na kumalizwa kabisa.”
Ameutaka Muhimili huo wa Mahakama kuzikabili changamoto zote ikiwemo kujiepusha na vitendo vya rushwa lakini pia waendelee kutoa elimu kwa umma na kuhakikisha elimu mbadala ya usuluhishi inapatikana na kuendeleza utaratibu wa maadhimisho ya kisheria ambayo yamekuwa yakitanguliwa na wiki ya sheria .
Maadhimisho hayo yalitanguliwa na maandamano kuanzia kituo Jumuishi cha Utoaji haki hadi uwanja wa Nyerere Square jijini Dodoma.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakani
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best