November 16, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mpango akemea vitendo vya uonevu, ukatili na unyanyasaji katika maeneo ya kazi

Na Jackline Martin

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango amekemea vitendo vya uonevu, unyanyasaji na ukatili katika maeneo ya kazi ambayo husababisha wafanyakazi kudhalilishwa na kuwa wanyonge mahali pa kazi hususani manyanyaso ya umri, jinsia, rangi, kabila, ulemavu pamoja na dini.

Makamu wa Rais aliyasema hayo wakati wa Hafla ya Utoaji Tuzo za Mwajiri Bora wa Mwaka 2022 zinazoratibwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) iliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam.

Alisema vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu na vinaathiri utendaji wa kazi sio tu kwa waathirika, bali kwa viongozi na Taasisi au Mashirika wanayofanyia kazi.

Aliongeza kwamba kila mfanyakazi ana haki ya kutendewa utu, kuthaminiwa na kuheshimika kazini na kuagiza kuwekwa mifumo itakayowezesha wafanyakazi kutoa taarifa za kunyanyaswa au kuonewa bila kuhofia madhara yoyote yanayoweza kujitokeza ikiwemo kupoteza ajira zao.

Halikadhalika Makamu wa Rais aliwasihi waajiri hapa nchini kuzingatia sheria na kutoa mikataba ya kazi kwa kazi zinazostahili mikataba badala ya kuwafanyisha watu kazi kama vibarua kwa kazi ambazo wangeweza kupata mikataba ya kazi.

Aidha aliiagiza Wizara ya Kazi kutoa elimu kwa waajiriwa kujua haki zao na pia kuhakiki aina ya mikataba inayotolewa ili ikidhi vigezo vyote muhimu ikiwa ni pamoja na kuainisha wajibu na haki za mwajiri/mwajiriwa kwenye masuala ya afya, likizo, ulemavu, mafao na migogoro.

Pia aliwasisitiza waajiri kuzingatia sheria zilizopo kuhusu ajira kwa wageni ikiwemo kuhakikisha nafasi zisizo za kitaalamu au ambazo utalaamu wake unaweza kupatikana hapa nchini hazitolewi kwa wageni.

Alisewasihi waajiri kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kulingana na tija yao katika uzalishaji ili waweze kujikimu kimaisha kulingana na wakati ikiwa ni pamoja na kutoa posho, tuzo na motisha mbalimbali ili kutambua mchango mkubwa wa wafanyakazi bora katika taasisi, kuwapandisha vyeo na kuwapatia stahili zinazoendana na nafasi zao.

Makamu wa Rais alIwataka kutumia tuzo hizo kuwa chachu ya kuboresha mazingira ya mahali pa kazi na kuhamasisha utendaji wenye tija kwa manufaa ya taasisi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Aidha, aliwahakikishia kuwa kupitia Serikali, Vyama vya Waajiri na Vyama vya wafanyakazi kuendelea kujadiliana masuala mbalimbali yanayohusu Ajira na Kazi nchini ili kuboresha na kutatua changamoto zilizopo kwa pamoja.

Alisema kwa upande wa Serikali chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imejipanga kuhakikisha sheria na sera za nchi zinakidhi mahitaji ya waajiri na waajiriwa.

Awali akimkaribisha Makamu wa Rais katika hadhara hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako alitoa wito kwa waajiri wa sekta binafsi kuzingatia kima cha chini cha mshahara kilichopangwa kuanza kutumika Januari 2023.

Alisema waajiri wanapaswa kutambua kwamba wafanyakazi ndio nguzo muhimu katika ufanisi wa shughuli wanazozifanya hivyo hawana budi kuwathamini.

Naye Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) Suzanne Ndomba alisema wataendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali za kuboresha mazingira ya ajira nchini hususa ni katika maeneo ya usawa wa kijinsia sambamba na usawa katika maeneo ya kazi.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akihutubia wakati wa Hafla ya Utoaji Tuzo za Mwajiri Bora wa Mwaka 2022 zinazoratibwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) iliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akikabidhi tuzo kwa Benki ya NMB ilioshinda kuwa Mwaajiri Bora wa Ujumla wa Mwaka 2022 wakati wa Hafla ya utoaji tuzo hizo zinazoratibwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) iliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam. (Kushoto ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Profesa Joyce Ndalichako na kulia ni Mwenyekiti wa Chama Cha Waajiri Tanzania (ATE) Bi. Jayne Nyimbo).
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango akiwa katika picha ya pamoja na washindi wa vipengele mbalimbali vya waajiri bora wa mwaka 2022 wakati wa Hafla ya utoaji tuzo hizo zinazoratibwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE) iliofanyika katika Ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es salaam.