Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdory Mpango, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuzindua Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond, inayolenga kukusanya kiasi cha Shilingi bilioni 150 kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya barabara za vijijini na mijini. Ujenzi huu utatekelezwa chini ya Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA).
Akimwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan, Dkt. Mpango amesema hayo katika hafla ya uzinduzi wa hatifungani hiyo, iliyofanyika jana katika Ukumbi wa Mlimani Ciity, jiji la biashara, Dar es Salaam na kuhudhuriwa na viongozi wa taasisi za umma na binafsi, wafanyabiashara, wawekezaji, na wananchi waliojitokeza kwa wingi kushiriki katika tukio hilo muhimu.
Akizungumza katika hafla hiyo, Dkt. Mpango alisema kuwa ni furaha kubwa kuona taasisi za kifedha za kizalendo zikiongoza juhudi za kuleta pamoja Watanzania na wawekezaji kutoka nje ya nchi kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya barabara, jambo ambalo litachochea maendeleo ya taifa kwa ujumla.
“Furaha yangu ya kujumuika katika masuala yanayochochea ustawi wa maendeleo ya taifa letu huwa maradufu ninapoona serikali, taasisi binafsi, na wananchi tunaungana kuijenga Tanzania yetu. Nafarijika sana ninapoona taasisi zetu zipo mstari wa mbele kuchochea maendeleo,” alisema Dkt. Mpango, akiongeza kuwa mradi huu utasaidia kuboresha miundombinu ya barabara, jambo muhimu kwa maendeleo ya uchumi.
Makamu wa Rais pia alisisitiza umuhimu wa hatifungani hii katika kuwashirikisha Watanzania wote na kusema kuwa kupitia mpango huu, serikali inapata shinikizo la kuhakikisha inajenga barabara nzuri na imara kadri inavyowezekana. Aliongeza kuwa ni jukumu la serikali kuhakikisha malipo kwa wakati kwa makandarasi, ili miradi yote iweze kutekelezwa kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, ameeleza kuwa benki hiyo inajivunia kuzindua hatifungani hii maalum kwa ajili ya miradi ya barabara, na kwamba kupitia hii, CRDB inatarajia kukusanya Shilingi bilioni 150 zitakazotumika kulipa makandarasi wanaoshiriki katika ujenzi wa barabara.
“Hatufungi hii itatoa fursa kwa kila Mtanzania kuwekeza, na tunatoa riba ya asilimia 12 kwa mwaka kwa wawekezaji, ambayo italipwa kila robo mwaka. Uwekezaji huu ni salama na wenye faida nzuri kwa wote wenye nia na uwezo wa kuwekeza,” alisema Nsekela, akibainisha kuwa wananchi wanaweza kununua hatifungani hii kwa kiwango cha chini cha Shilingi 500,000, na kwamba uwekezaji huo unaweza kufanywa kwa njia ya kidijitali kupitia SimBanking.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), CPA Nicodemus Mkama, alieleza matumaini yake kwamba mauzo ya Samia Infrastructure Bond yatavuka malengo yaliyokusudiwa, kama ilivyotokea katika awamu ya kwanza ya mauzo ya Hatifungani ya Kijani, ambayo ilikusanya Shilingi bilioni 171.82, zaidi ya mara nne ya malengo.
“Wananchi wameshajitokeza kuwekeza kwenye masoko ya mitaji na dhamana, na naamini rekodi ya awali itavunjwa. Huu ni muda muafaka kwa Watanzania kuwekeza kwenye fursa hii ya miundombinu,” alisema Mkama.
Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa, alisisitiza kuwa Benki ya CRDB ndiyo taasisi pekee inayokwenda sambamba na matakwa ya wizara katika kutafuta vyanzo mbadala vya fedha kwa ajili ya ujenzi wa barabara. Alipongeza juhudi za benki hiyo na kusema kuwa miradi ya barabara itakamilika kwa wakati na kwa ubora, ikiwa fedha zitapatikana kwa wakati.
Afisa Mtendaji Mkuu wa TARURA, Mhandisi Victor Seff, aliongeza kuwa ushirikiano huu na CRDB utasaidia kuboresha utekelezaji wa miradi ya barabara nchini. Alisisitiza kuwa hatifungani hii ni fursa kubwa kwa Watanzania kuwekeza katika maendeleo ya miundombinu ya barabara na kuhimiza makandarasi kutekeleza kazi zao kwa viwango vinavyokubalika.
Kwa kumalizia, Dkt. Mpango alisisitiza kuwa uzinduzi wa Samia Infrastructure Bond ni sehemu ya jitihada za serikali za kuhakikisha kuwa Tanzania inakuwa na miundombinu ya kisasa inayochochea maendeleo ya uchumi. Aliwahimiza Watanzania, taasisi, na wawekezaji kujiunga katika mchakato huu wa kujenga barabara, na kwa pamoja kutimiza malengo ya maendeleo ya taifa.
Hatifungani ya Samia Infrastructure Bond itakuwa wazi kwa uwekezaji kuanzia tarehe 29 Novemba 2024 hadi 17 Januari 2025, na inatoa fursa kwa kila Mtanzania kuwekeza katika miradi ya barabara inayojengwa na Watanzania wenyewe.
More Stories
Mwinyi: Kuna ongezeko la wawekezaji Zanzibar
Othman awakabidhi jezi Zanzibar Heroes
Maofisa Watendaji watakiwa kufanya kazi kwa weledi