December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mpango aagiza kuchukuliwa hatua waliokwamisha ujenzi wa Hospitali

Na Allan Vicent, TimesMajira Online Tabora

SERIKALI imemwagiza Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya manispaa Tabora na Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoani hapa kuhakikisha waliokwamisha ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo wanachukuliwa hatua mara moja.

Agizo hilo limetolewa jana na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Phillip Isdor Mpango alipotembelea hospitali hiyo ili kujionea hali ya utoaji huduma kwa wananchi.

Alisema ujenzi wa hospitali hiyo ni moja ya utekelezaji wa ahadi zilizotolewa na Mheshimiwa Rais Dkt Samia Suluhu Hassan lakini akasitishwa na kitendo cha baadhi ya watumishi wa halmashauri hiyo kukwamisha mradi huo pasipo sababu.

‘Nataka hospitali hii ikamilike haraka ili Mheshimiwa Rais aje kuizindua, najua imejengwa kwa muda mrefu na ina mapungufu mengi lakini waliosababisha mapungufu hayo hadi sasa hawajachukuliwa hatua yoyote’, alieleza.

Dkt Mpango alisisitiza kuwa ujenzi wa hospitali hiyo haukupaswa kucheleweshwa kwa muda wote huo hivyo akamwagiza Mkuu wa Mkoa, Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri na Uongozi wote kuchukua hatua za haraka ili mradi huo ukamilike.

Alibainisha kuwa mradi huo umegubikwa na upigaji mwingi hivyo akamwagiza Mkuu wa TAKUKURU na Mkurugenzi wa halmashauri hiyo kuhakikisha wale wote waliohusika na ubadhirifu wa fedha za mradi huo wanafikishwa mahakamani, aliwataka kumpa majibu ndani ya siku 30 za hatua iliyochukuliwa.

Alitoa wito kwa watoa huduma za afya wote wakiwemo wauguzi na madaktari kuzingatia viapo vya kazi zao na kutumia taaluma zao kuokoa maisha ya wananchi ikiwemo kujiepusha na mambo yanayokwaza jamii.

Aliwahakikishia kuwa serikali itaendelea kutekeleza ahadi zake kwa wananchi ikiwemo kutenga fedha zaidi ili kuboresha miundombinu ya hospitali zilizojengwa katika wilaya zote nchini.

Wakati huo huo Makamu wa Rais ameagiza wakazi wa manispaa hiyo na mikoa yote nchini kulinda uoto wa asili usiharibiwe ili kuepusha uharibifu wa mazingira yao huku akisisitiza kila kaya kuwa na sehemu ya kuchomea taka.

Kuhusu kuongezeka kwa matukio ya mauaji katika mkoa huo, Dkt Mpango alisisitiza kuwa ni marufuku mtu yeyote kujichukulia sheria mkononi hivyo akashauri viongozi wa dini, mila, chama na serikali washirikishwe ili kukomesha tabia hiyo. 

Awali akitoa taarifa ya mradi huo Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo Dkt Peter Nyanja alisema mradi huo umeshagharimu kiasi cha sh bil .3 hadi sasa na hadi kukamilika kwake unatarajiwa kugharimu kiasi cha sh bil .8.

Alibainisha kuwa huduma za afya tayari zinaendelea kutolewa katika hospitali hiyo baada ya kukamilika kwa ujenzi wa baadhi ya wodi ikiwemo jengo la mama na mtoto.

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani hapa Mussa Chaulo alimweleza Makamu wa Rais kuwa uchunguzi wa mradi huo ulishafanyika na kubaini mapungufu makubwa katika suala la manunuzi ya vifaa vya mradi na tayari jalada la uchunguzi limeshapelekwa kwa Mwendesha Mashtaka wa serikali kwa hatua zaidi.

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI alimhakikishia Makamu wa Rais kuwa watafanyia kazi maelekezo yote aliyoyatoa kuhusiana na mapungufu yaliyobainika katika mradi huo na wote watakaobainika kuhusika sheria itachukua mkondo wake.