Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online, Kagera
NAIBU Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel ametoa wito kwa Wadau na watendaji wote wa Serikali kuhakikisha fedha zote zinazoingia nchini na zinazotoka Serikalini kupitia ziara za nje za Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan zikatatue changamoto zilizokusudiwa za wananchi katika vijiji kuliko kwenye semina na warsha.
Dkt. Mollel ametoa wito huo leo Agosti 07, 2023 wakati akizindua kampeni ya ugawaji wa vyandarua katika maeneo yote ya mikoa ya Kagera na Tabora inayoambatana na elimu itayosaidia katika mapambano dhidi ya maambukizi ya Ugonjwa wa Malaria katika mikoa hiyo.
“Niwaasa taasisi zote za Serikali na zisizo za Serikali, Rais wetu anapoenda kuzunguka kwenda kwenye makampuni makubwa na mashirika makubwa duniani ili kutafuta fedha, vipaumbele vyake ni kwenda kumfikia Mtanzania mnyonge kutatua changamoto katika vijiji”.Amesema Dkt. Mollel.
Sambamba na hilo, Dkt. Mollel amewataka Wadau kupunguza semina, warsha na mafunzo na fedha hizo ambazo zimetumika huko zielekezwe katika kuongeza nguvu kutatua changamoto zinazowagusa Watanzania wenye uhitaji ikiwemo changamoto za afya.
Aidha, Dkt. Mollel ametoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Kagera kutumia vyandarua vilivyo na dawa na kusikiliza vizuri maelekezo na ushauri kutoka kwa Wataalamu wa afya hasa kwenye afua mbalimbali za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria ili kufanikisha dhamira ya Serikali ya kuutokemeza ugonjwa huo nchini.
Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Erasto Sima ameomba Serikali kupitia Wizara ya Afya kuupa Mkoa wa Kagera kipaumbele kwenye eneo la rasilimali fedha na watu ili kuhakikisha wanatokomeza ugonjwa wa Malaria kwani Mkoa huo ni moja kati ya mikoa inayoongoza kuwa na maambukizi ya Ugonjwa wa Malaria.
Pia, amewashauri wananchi kujenga tabia ya kupima ugonjwa wa Malaria kabla ya kutumia dawa ili kuondoa usugu wa dawa, huku akibainisha kama mkoa wataendelea kutekeleza juhudi za mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria ikiwemo kusafisha mazingira na kutoa elimu ya mapambano dhidi ya ugonjwa huo.
Nae, Mkurugenzi wa afya ,Ustawi wa jamii na lishe OR-TAMISEMI Dkt. Ntuli Kapologwe amesema kama wasimamizi wa Sera watahakikisha Halmashauri zote zinatekeleza ununuzi wa viududu kupitia kiwanda cha Kibaha kwani tayari TAMISEMI imetenga bajeti kwaajili ya ununuzi wa viuadudu hivyo kwenye Halmashauri zote nchini.
More Stories
Waziri Jerry afanya uteuzi wa Makamu Mwenyekiti, Wajumbe watano wa bodi ya Shirika la Posta
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa