Na WAMJW- Arusha.
Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Godwin Mollel amefanya ziara katika mpaka wa Tanzania na Kenya, Namanga Jijini Arusha na kuzungumza na madereva wa malori yanayokwenda Kenya ili kusikiliza changamoto zinazowakumba.
Dkt. Mollel amefanya ziara hiyo leo, ikiwa ni sehemu ya kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazowakumba madereva hao, katika kipindi hiki ambacho Dunia imekumbwa na maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya Corona.
Amesema, Serikali imeliona tatizo hilo na itaongeza kasi katika kuhakikisha inapata suluhu ya changamoto wanazokumbana nazo madereva hao katika eneo la mpaka wa Namanga.
Dkt. Mollel amesema, changamoto hiyo iliyojitokeza katika mpaka wa Namanga ni suala mtambuka ambalo linahusisha Wizara zaidi ya moja, huku akiweka wazi kuwa suala hilo lina uhusiano wa kibiashara na uchumi baina ya nchi hizo.
“Nimekuja kuwapa pole, lakini Serikali yetu itaenda kwa kasi ya ajabu kuhakikisha hili tatizo lenu katika mpaka huu linatatuliwa hivyo nawaomba muendelee kuwa wavumilivu kipindi hiki ambacho, Serikali inatafuta utatuzi wa changamoto na wanaomba mpokee salamu kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli kuwa anawapenda sana,” amesema Dkt. Mollel.
Mmoja wa madereva wa malori yanayokwenda nchini Kenya, Abdullah Hassan amesema, kama madereva hawakubaliani na majibu ya vipimo wanavyopewa kutoka Kenya kutokana na vipimo hivyo kuonesha idadi kubwa ya madereva kuwa na ugonjwa wa Corona jambo ambalo sio kweli.
“Tunaishi maisha magumu sana kutokana na hali iliyojitokeza, na kunachosikitisha zaidi, sisi hatukubaliani na vipimo ambavyo tunapimwa upande wa pili”.
Japhet Jeremiah amesema, wamekuwa wakiombwa kiasi cha shilingi 2000 za Kenya ili kuandikiwa kuwa hawana Corona, jambo ambalo ni wazi kuwa ni uonevu kwa madereva kutoka Tanzania ambao hadi wanafikia hatua ya kugoma.
More Stories
Kapinga atoa maagizo TANESCO ,kuhusu Vijiji vinavyolipia gharama ya mijini kuunganisha umeme
Ukiukaji wa Uhuru wa Kidini na Kutovumiliana Huzusha Malumbano ya Kimataifa
NLD kipo tayari kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa