November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Maguo:chuo kikuu huria kimetoa watu mahiri akiwemo Rais Samia

Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online, Dar es Salaam

MKURUGENZI Mkuu wa Mawasiliano na Masoko wa Chuo Kikuu Huria (Open University), Dkt. Mohammed Maguo, amesema kuwa chuo hicho kimetoa watu wengi mahiri akiwemo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye alisoma Master of Community Economic Development.

Huku akiwatoa hofu wanafunzi waliofanya vibaya katika masomo yao ya elimu ya sekondari, kujiunga na chuo hicho kwa kuanza ngazi ya chini yani (Foundation).

Dkt. Maguo amesema hayo jana katika ufunguzi wa maonesho ya 18 ya Vyuo Vikuu, yanayoendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam na kufunguliwa na Waziri wa Elimu, Prof. Adolf Mkenda.

Amesema, chuo hicho kinatoa huduma mbalimbali kuanzi ngazi ya cheti (Certificate) hadi Shahada ya Udhamivu (PHD), ambapo amesema kuwa kwa wanafunzi ambao wamemaliza kidato Cha sita hivi karibuni na kufanya vibaya, wanaweza kujiunga na chuo hicho kwa ngazi ya ‘Foundation’ kwa mwaka mmoja na hapo baadae kuweza kujiunga na vyuo vingine kwa kozi mbalimbali ikiwepo chuo hicho.

“Tunapenda kukaribisha wanafunzi wote waliomaliza kidato sita hivi karibuni kujiunga na bachelor degree ambayo tunatoa katika chuo chetu, lakini pia tunakaribisha wale wote ambao wamepungukiwa kidogo katika ufaulu wao waje na wataanza ngazi ya chini ya foundation na diploma,” amesema Dkt. Maguo.

Dkt. Maguo ametoa wito kwa wananchi wote kufika katika banda la chuo hicho, katika maonesho hayo ili kuweza kujua mambo mbalimbali ikiwa pamoja na kujua kozi zinazotolewa na chuo hicho ili kuweza kuwarahisishia katika uombaji wao.