December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mamia ya wakazi wa Kata ya Tinde wilayani Shinyanga wakimsikiliza mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli (hayuko pichani) aliposimama kwa muda katika kata hiyo kuwasalimia wananchi hao ambapo pia aliwaomba wampe kura za kishindo ifikapo Oktoba 28, mwaka huu. (Picha na Suleiman Abeid)

Dkt.Magufuli awatoa hofu wagombea Ubunge waliokatwa CCM

Na Suleiman Abeid,TimesMajira,Online Shinyanga

MGOMBEA Urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dkt. John Magufuli amewataka wanachama wa CCM waliotia nia ya kugombea ubunge na kushindwa kuteuliwa waache kubabaika na badala yake watulie kwa vile ana uhakika zipo kazi nyingine anazoweza kuwapatia.

Dkt. Magufuli ametoa kauli hiyo wakati akiwasalimia wakazi wa Kata ya Tinde wilayani Shinyanga akiwa njiani kuelekea mjini Shinyanga akiendelea na kampeni za kuomba kura kutoka kwa wakazi wa mkoa huo ambapo amewataka wana CCM kuheshimu maamuzi ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa (NEC).

Amesema hakuna sababu za wana CCM kupingana na maamuzi ya NEC kutokana na uteuzi walioufanya kwa vile wanaelewa fika kila aliyeteuliwa ana uwezo wa kufanya kazi vizuri na wale ambao hawakupata nafasi mfano wa wabunge wa majimbo ya Msalala wilayani Kahama, Ezekiel Maige na Stephen Masele Shinyanga Mjini anaweza kuwapatia kazi nyingine za kufanya.

Amesema ndani ya Serikali kuna kazi nyingi za kufanya ambapo alitoa mfano wa ubalozi katika nchi za nje na kwamba hakuna sababu za watu kubabaika kwa kukosa kuteuliwa ubunge kwa vile yeye anaamini nafasi anazo nyingi hata ukuu wa mkoa.

“Ndugu zangu tuache kulalamika, tukipiganie Chama chetu kiweze kushinda katika nafasi zote tatu, udiwani, ubunge na urais, na hapa Solwa niliteeni Ahmed Salum, msinichanganyie na wale wa upinzani, hapa tunahitaji mtu wa CCM, hatuhitaji sura ya mtu, mkinichagua mimi ndiyo nitakuwa Rais,”

“Nataka niwaambie ukweli nikiwa Rais, mnafikiri nitaacha kumpa kazi Masele (Stephen), siwezi kumuacha hivi hivi nawaeleze hivi sababu sisi CCM tunafahamu, lakini pia maamuzi ya NEC lazima yaheshimike, kwamba tukimleta huyu atatuleta hapa, siyo Shinyanga tuwe tunashinda kwa kura moja, hapana,” ameeleza Dkt. Magufuli.

Mgombea huyo amekemea makundi ndani ya CCM na kwamba ndani ya CCM hakuna ubaguzi wa aina  yoyote bali wote ni kitu kimoja hivyo hakuna sababu za watu kuchukia kwa vile tu mtu waliyekuwa wanamuunga mkono hakuchaguliwa kugombea iwe udiwani ama ubunge.





 
Baadhi ya viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Shinyanga wakisubiri kumpokea mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Magufuli katika eneo la Kata ya Tinde wakati akitokea mkoani Tabora ambapo leo Alhamisi anatarajiwa kuhutubia mkubwa wa kampeni utakaofanyika kwenye viwanja vya CCM Kambarage. (Picha na Suleiman Abeid


Kwa upande mwingine Dkt. Magufuli ameahidi kuongeza idadi ya madaktari na wauguzi katika Kituo cha Afya cha Tinde baada ya kulikubali ombi lililotolewa na mgombea udiwani katika kata ya Tinde Jaffari Kanola.

Awali mgombea ubunge katika Jimbo la Solwa, Ahmed Salum alimshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa kulipatia jimbo hilo fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, afya na miundombinu ya barabara na kwamba ndani ya kipindi cha miaka mitano cha uongozi wake kero nyingi za wananchi wa Jimbo la Solwa zimepatiwa utatuzi.