April 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Mabula:Kero za msingi Ilemela zinahitaji uboreshaji

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online – Dodoma

Dkt. Anjelina Mabula: Serikali Imekuwa Mchapa Kazi, Lakini Zipo Kero za Msingi Zinazohitaji Uboreshaji

Mbunge wa Jimbo la Ilemela, Dkt. Anjelina Mabula amepongeza juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hasa katika kuboresha huduma za kijamii ambazo zimekuwa mkombozi mkubwa kwa wananchi wa maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza Bungeni jijini Dodoma Aprili 22,2025 wakati akichangia bajeti ya Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI)kwa mwaka 2025/2026, Dkt. Mabula amesema Rais ametenda haki kubwa kwa Wizara ambazo zinahusiana moja kwa moja na maisha ya wananchi, hivyo kustahili pongezi kwa mafanikio hayo.

Wenyeviti wa Mitaa na Mabalozi: Wafanya Kazi Kubwa Bila Haki Stahiki

Mbunge huyo alieleza kuwa pamoja na maendeleo hayo, bado kuna changamoto kubwa zinazowakabili wenyeviti wa Serikali za Mitaa na mabalozi ambao ni kiungo muhimu katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo.

“Wenyeviti wa mitaa wanapokea posho ya shilingi 20,000 tu, jambo ambalo si haki ikilinganishwa na majukumu wanayoyatekeleza. Serikali iangalie uwezekano wa kuwapatia kiinua mgongo cha angalau milioni 3 hadi 5 baada ya kumaliza muda wao wa miaka mitano,” alisema Dkt. Mabula.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kutambua mabalozi kisheria kwa sababu wanatoa mchango mkubwa katika maendeleo ya jamii, lakini hadi sasa wanatambulika kupitia vyama vya siasa tu.

TARURA: Hongera Zatolewa, Lakini Bajeti Isawazishwe

Katika hotuba yake, Dkt. Mabula alimpongeza Mkurugenzi Mkuu wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), Mhandisi Rogatus Seif, kwa usikivu na mshikamano wake na wananchi. Hata hivyo, alieleza kutoridhishwa na mgawanyo wa bajeti katika baadhi ya halmashauri.

“Tukiangalia kwa mfano, Manispaa ya Ilala inapata shilingi bilioni 29, wakati Ilemela yenye mtandao wa barabara wa kilometa 1,920 inapata bilioni 3 tu. Hii haileti uwiano wa maendeleo,” amesema.

Mbunge huyo alikumbusha ahadi ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan aliyotoa Januari 30, 2024 ya kujenga kilometa 12 za lami katika jimbo hilo, ambayo hadi sasa haijatekelezwa, na kuomba TAMISEMI, Wizara ya Fedha na TARURA kuhakikisha ahadi hiyo inakamilishwa.

Uboreshaji wa Miundombinu na Miradi ya Kimkakati

Akizungumzia maendeleo ya miji, Dkt. Mabula amesema Manispaa ya Ilemela imepata fursa ya kutekeleza miradi mikubwa kama ujenzi wa soko la Kimataifa la Kirumba na barabara za lami kilometa 2.9. Alishukuru Serikali kwa kulipa mkandarasi na kuonesha matumaini ya kurejea kwake site.

Aidha, alilalamikia ucheleweshwaji wa utekelezaji wa miradi ya Green Smart Cities ikiwemo mialo ya Kirumba, Igombe na Old Gold ambayo upembuzi wake ulifanyika tangu 2022 lakini utekelezaji haujaanza hadi leo.

“Wilaya yangu asilimia 77 ni maji, asilimia 23 ni nchi kavu. Uchumi wa Ilemela unategemea uvuvi. Hili ni eneo la kimkakati linalostahili kupewa kipaumbele,” alisisitiza.

Stendi ya Inyamanolo na Changamoto za Matumizi

Dkt. Mabula aliipongeza Serikali kwa mradi wa stendi ya Inyamanolo ambayo ni ya kisasa na ina huduma mbalimbali kama hoteli, sehemu za malori na mizigo. Hata hivyo, alieleza kuwa stendi hiyo haitumiki ipasavyo kama ilivyokusudiwa.

Machinga na Mikopo kwa Makundi Maalum

Kuhusu wafanyabiashara wadogo (wamachinga), Dkt. Mabula alisema utekelezaji wa agizo la Serikali kwa Halmashauri kutenga maeneo bado haujaeleweka vizuri, jambo linalowaacha wamachinga wakihangaika bila pa kwenda.

Katika mikopo ya makundi maalum, alitoa wito kwa Serikali kuangalia upya elimu ya mikopo pamoja na masharti ya utoaji wake kwani bado yanawabana wengi.

“Mfanyabiashara anayefahamika na ana biashara, apewe mkopo kama mtu binafsi. Hakuna haja ya kulazimishwa kuunda kikundi ambacho siyo imara,” amesema.

Mbunge huyo aliendelea kuhimiza Serikali kuangalia maeneo yenye changamoto na kuyapa kipaumbele ili kuhakikisha maendeleo ya kweli yanawafikia wananchi wote kwa usawa. Alisisitiza kuwa maendeleo hayawezi kufikiwa bila kuwahusisha viongozi wa ngazi za chini wanaofanya kazi kubwa kwa kujitolea.