January 10, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Mabula asikitishwa wananchi kutochangamkia hati zoezi la urasimishaji Ubungo

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameonesha kutorishwa na kasi ya wananchi wa wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam kutochangamkia fursa ya kupatiwa hati kupitia zoezi la urasimishaji makazi holela.

Hali hiyo imejitoleza wakati wa utoaji hatimiliki za ardhi kwa wananchi 1081 wa maeneo tofauti wilayani ubungo waliokamilisha taratibu za kumilikishwa ardhi kupitia zoezi la urasimishaji makazi holela tarehe 20 Desemba 2022 eneo la Stop Over kata ya Saranga Dar es Salaam.

Huku akieleza kupitia takwimu za zoezi la urasimishaji katika wilaya ya Ubungo, Dkt Mabula alisema kazi kubwa imefanywa na ofisi ya ardhi halmashauri ya Ubungo ambapo hatimiliki 1081 zimekamilishwa na kugawiwa kati ya viwanja 23,967 vilivyopimwa na kuidhimishwa.

“Wote waliotimiza wajibu wao hakuna hati inayodaiwa hapa. Wapo waliotimiza wajibu na hawaendi kuchukua sasa unataka serilali ifanye nini? alihoji Waziri wa Ardhi Dkt Angeline Mabula.

Kwa mujibu wa Dkt Mabula, changamoto ya zoezi  urasimishaji  makazi holela ipo pande zote mbili za wananchi na makampuni yanayofanya kazi za urasimishaji na kusema kuwa haiwezekani hati 1081 pekee ndiyo zikamilishwe na kugawiwa wananchi kati ya viwanja 23 967 vilivyoidhinishwa.

“Haiwezekani Ubungo idadi ya vipande vya ardhi vilivyotambuliwa ni 182, 215 kutoka michoro 520. Idadi ya vowanja vilivyopangwa na kuidhinishwa ni 177,325. Idadi ya viwanja  vilivyowekewa bicon  76,250. Vilivyopimwa na kuidhinishwa ni 23,967. Ankara zilizotoka 4338, idadi ya maombi ya hati 7164, idadi ya hati zilizotolewa 6,885 na leo kuna hati 1,081 ukijumlisha hapo maana yake hakuna hati inayodaiwa katika ofisi ya ardhi” alisema Dkt Mabula.

Amesema, kwa wale wote waliotimiza wajibu wao hakuna hati inayodaiwa mpaka wanakwenda kutekeleza zoezi la kugawa hati wilayani Ubungo lakini wapo wale wananchi waliotimiza wajibu wa kulipa na kuandaliwa hati lakini hawaendi kuchukua na kuhoji hapo serikali ifanye nini na kunainisha kuwa ilichoamua wizara yake ni kuwafuata walipo kwa lengo ni kuhakikisha hakuma wanachodai ndani ya wizara.

Kwa upande wake Mbunge wa jimbo la Kibamba Issa Mtemvu pamoja na kuelezea kuendelea vizuri kwa zoezi la urasimishaji makazi holela kwa baadhi ya kata za jimbo lake na kuzitaja Saranga, Ukombozi na Mpakani  lakini baadhi ya wananchi wanakabiliwa na changamoto za malipo ya kukamilisha ili kupatiwa hati na kuiomba wizara kuangalia namna ya kuwasaidia ili waweze kupatiwa hati.

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akizungumza na wananchi wa wilaya ya Ubungo mkoani Dar es Salaam wakati wa zoezi la utoaji hati kwa wananchi wa wilaya hiyo lililofanyika eneo la Stop Over tarehe 20 Desemba 2022.
 
Sehemu ya wananchi wa wilaya ya Ubungo waliojitokeza kumsikiliza Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula wakati wa zoezi la utoaji hati kwa wananchi wa wilaya hiyo waliokamilisha taratibu za kupatiwa hati katika zoezi la urasimishaji makazi holela tarehe 20 Desemba 2022.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula akimkabidhi hati mkazi wa wilaya ya Ubungo mkoa wa Dar es Salaam wakati wa zoezi la utoaji hati kwa wananchi wa wilaya hiyo waliokamilisha taratibu za kupatiwa hati katika zoezi la urasimishaji makazi holela tarehe 20 Desemba 2022
Mbunge wa jimbo la Ubungo Kitila Mkumbo akizungumza wakati wa zoezi la utoaji hati kwa wananchi wa wilaya hiyo waliokamilisha taratibu za kupatiwa hati katika zoezi la urasimishaji makazi holela tarehe 20 Desemba 2022.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na wabunge wa wilaya ya Ubungo Kitila Mkumbo-Ubungo (Kulia) na Issa Mtemvu-Kibamba (Kushoto) wakati wa zoezi la utoaji hati kwa wananchi wa wilaya hiyo waliokamilisha taratibu za kupatiwa hati katika zoezi la urasimishaji makazi holela tarehe 20 Desemba 2022.Â