January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Kiruswa atatua mgogoro wa wachimbaji Longido

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Arusha

NAIBU Waziri wa Madini Dkt.Steven Kiruswa ametatua mgogoro wa wachimbaji wadogo wa Madini ya Ruby Wilaya ya Longido Mkoani Arusha uliodumu zaidi ya miaka mitano kati ya Kampuni ya Paradiso Mineral (T) Limited na Mzee Malulu Ole Moringo kwa Kampuni hiyo kukubali kumlipa fidia Mzee Malulu Ole Moringo ya jumla ya shillingi milioni miamoja na hamsini ili kupisha shughuli za uchimbaji madini.

Makubaliano hayo yameafikiwa leo Disemba 6,2024 wakati Dkt. Kiruswa alipofanya ziara ya kutatua mgogoro huo katika Kata ya Mundarara Wilaya ya Longido Mkoani Arusha.

Dkt.Kiruswa ameielekeza kampuni ya Paradiso kutekeleza makubaliano walioafikiana na Mzee Malulu Ole Moringo ya kulipa fidia hiyo kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza wanatakiwa kulipa milioni 100 ifikapo Januari 30, 2025 na milioni 50 ifikapo Machi 30, 2025.

Aidha,Dkt.Kiruswa amesisitiza makubaliano hayo kutekelezwa kwa wakati na endapo kampuni ya Paradiso itakiuka makubaliano hayo Serikali itachukua hatua za kisheria ikiwemo kusimamisha shughuli za uchimbaji katika eneo hilo.

Sambamba na hayo, Dkt. Kiruswa amesema Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na  Dkt. Samia Suluhu Hassan haitaki migogoro katika sekta ya Madini ili sekta hiyo kuwa na  maendeleo.

Pamoja na mambo mengine,Dkt.Kiruswa amewataka wachimbaji wa madini kuendelea kulipa kodi za Serikali ambapo fedha hizo zitakwenda kuboresha huduma za kijamii kama vile kujenga shule na usambazaji wa umeme maeneo mbalimbali hapa nchini.

Awali,Ofisi ya Madini Arusha ilifanya utafiti na kugundua Malulu Ole Moringo ana haki katika eneo hilo ambalo familia ya Jango Master inafanya shughuli za uchimbaji Madini.

Kwa upande wake,Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Mkoa wa Arusha (CCM) Papaanakuta Moleli amempongeza Dkt. Kiruswa kwa kazi nzuri anazozifanya za kutatua migogoro mbalimbali ya wachimbaji wa Madini  hapa nchini.

Nayo, Familia ya Jango Master ikiwakilishwa na Victor Jango imekubali kulipa fidia hiyo kwa wakati, huku Malulu Ole Moringo naye akiridhia kupokea fidia hiyo kama Serikali ilivyoelekeza.