November 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Kijaji akutana na WTTC kuhusu uhifadhi na uwekezaji nchini

Na Mwandishi Wetu,TimesMajira

WAZIRI wa Maliasili na Utalii,Dkt. Ashatu Kijaji, leo Novemba 8, 2026, amekutana na kufanya mazungumzo na Mwenyekiti wa Baraza la Utalii na Usafiri Duniani (WTTC), Manfredi Lefebvre, katika Hoteli ya Hyatt jijini London, Uingereza.

Mazungumzo hayo yamejikita katika masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano katika sekta ya utalii, hususan uwekezaji katika maeneo ya hifadhi pamoja na kuongeza idadi ya watalii wanaotembelea Tanzania.

Katika kikao hicho, pande hizo zimejadili fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali ya hifadhi nchini, yakiwemo Hifadhi ya Taifa ya Nyerere, Serengeti na maeneo mengine yenye vivutio vya kipekee vya utalii, kwa lengo la kuimarisha huduma za utalii na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika uchumi wa Taifa.

Lefebvre, ambaye pia ni mmiliki wa kampuni ya kimataifa ya utalii ya Abercrombie & Kent, ni miongoni mwa wawekezaji wenye maslahi na shughuli za utalii nchini Tanzania.

Kupitia uwekezaji na shughuli zake za utalii wa kimataifa, ikiwemo huduma za meli za kitalii za Crystal Cruises, Tanzania imeendelea kunufaika na ujio wa maelfu ya watalii wanaotembelea maeneo mbalimbali nchini, yakiwemo Zanzibar, Kilwa na Dar es Salaam.

Mkutano huo ni sehemu ya mwendelezo wa ziara ya Waziri Dkt. Kijaji nchini Uingereza, yenye lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa, kuvutia uwekezaji na kuitangaza Tanzania kama kituo kinachotoa fursa mbalimbali za utalii na uhifadhi.

Kikao hicho kimehudhuriwa pia na Balozi wa Tanzania nchini Uingereza Mbelwa Kairuki, Naibu Kamishna wa Uhifadhi katika Mamlaka ya Hifadhi ya Eneo la Ngorongoro Joas Mwakwati na Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Utalii Tanzania, Dkt. Thereza Mugobi.