December 26, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt Kijaji aitaka NDC kuharakisha ulipaji fidia kwa wananchi Njombe

Na David John,Timesmajira Online,Dar es Salaam

WAZIRI wa Viwanda na Biashara Dkt.Ashatu Kijaji amelitaka Shirika la Maendeleo ya Taifa(NDC),kuharakisha mchakato wa ulipaji fidia kwa wananchi wanaotakiwa kuachia maeneo ili kupisha utekelezaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma wilayani Ludewa mkoani Njombe.

Dkt.Ashatu ameeleza kuwa NDC inatakiwa hadi
kufikia Septemba 24 mwaka huu wawe wamekamilisha zoezi la ulipaji wa fidia ili kuanza utekeleza wa mradi huo kwani Rais Samia Suluhu Hassan aliridhia kutoa kiasi cha biilioni 15 .4 za kitanzania kwa ajili ya kuwalipa fidia wananchi wanaotakiwa kuachia maeneo hayo.

Waziri Dkt.Ashatu Kijaji akizungumza katika hafla fupi ya kushuhudia utiaji saini ya kuanza kwa utekelezaji wa mradi wa kuzalisha makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma wilayani Ludewa Mkoa wa Njombe.

Waziri huyo ameyasema hayo jijini Dar es Salaam katika hafla fupi ya kushuhudia utiaji saini kwa kampuni tano za wazawa ambazo zimepewa dhamana ya kuchimba madini hayo ya makaa ya mawe ya Liganga na Mchuchuma mkoani Njombe .

“Hii ni dhamira ya dhati na ya hali ya juu ya Serikali ya awamu ya sita ya kuhakikisha ndoto za utekelezaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma zinatimia na rasilimali hizi ambazo zimekaa kwa muda mrefu bila kuwanufaisha wananchi ziwanifaishe na kuchangia katika uchumi wa nchi,”amesema Dkt.Kijaji.

Aidha ameeleza kuwa kwa nyakati tofauti Rais Samia amekuwa akisema kuwa ni wakati sasa umefika kwa rasilimali iliyopo katika miradi ya kimkakati ya Liganga na Mchuchuma kuanza uzalishaji na kwamba ni shauku yake kuona mradi huo wa muda mrefu unatekelezwa.

Pia katika hatua nyingine Waziri Dkt.Ashatu amewataka wawekezaji waliofanikiwa kusaini mikataba ya uchimbaji madini hayo kuhakikisha wanaaza shughuli za uchimbaji kwa haraka na kufikia kiwango walichokubaliana cha tani 30 kwa mwezi ambapo wawekezaji hao wanamiliki vitalu vitano kwa maana kila mmoja kitalu kimoja.

” Mwekezaji atakayeeshindwa kuaza kuchimba kwa muda tuliokubaliana basi atatupisha ili Serikali impe mwekezaji mwingine kwa maana waliokuwa wameomba kwenye mradi huo walikuwa 25 hivyo wapo stendi bai kwaio jambo la msingi kwenu nikuaza kazi tu,”amesema Waziri huyo.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mwendeshaji wa NDC Dkt. NIcolaus Shombe,amesema awali mchakato huo ulihusisha jumla ya kampuni 25 kati ya hizo 17 zilifanikiwa kuwasilisha maombi yao kwa ajili ya uchambuzi na ushindani na hatimaye zilipatikana kampuni tano zilizokidhi vigezo .

Alitaja kampuni hizo kuwa ni Sheby Mix investment limited .Nipo Engineering limited .Chusa Mining Company limited .Kindaini Company limited .na Cleveland Mine Service Company limited na mkataba huo utadumu Kwa miaka mitano.

Mkurugenzi Mwendeshaji wa Shirika la Maendeleo la Taifa NDC NIcolaus Shombe kulia akikabidhi kitabu cha saini ya makubaliano kwa mmoja wa mwekezaji kwenye mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao unakwenda kuaza uchimbaji hivi karibuni .

Naye Mkurugenzi wa kampuni ya Cleveland Mine services Company Ndaisaba Ruhoro alimpongeza Rais Samia kwa kuwaamini wao kama wazawa na kuhaidi kutomwangusha .

Amesema mara kadhaa imezoeleka miradi mikubwa kama hiyo wanapewa wageni kutoka nje ya nchi lakini katika kuhakikisha wazawa wanaweza wakikidhi vigezo leo wameaminiwa na wanakwenda kutekeleza mradi huo kama kampuni za kizawa.

Mkurugenzi wa kampuni ya Cleveland Mine Services Company Limited .Ndaisaba Ruhoro akikabidhiwa kitabu cha saini ya makubaliano kuhusu utekelezaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma Ludewa

Hivyo ameiomba Serikali ikiwapendeza basi wanaweza kuona namna ya kuwaongezea vitalu vingine kwa sababu wanauwezo wakuchimba zaidi ya tani 30 walizopewa na Serikali Kwa mwezi.