May 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Jafo:Fufueni viwanda kabla serikali haijaingiza mkono wake

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

WAZIRI wa Viwanda na Bishara Dkt.Selemani Jafo amewataka wote walipata viwanda na havifanyikazi wavifufue kwa hiyari yao kabla ya Serikali haijaingiza mkono wake.

Amesema kuwa serikali inampango wa miaka sita ya ujenzi wa viwanda wenye lengo la kujenga viwanda 948,000 ambapo ndani yake kuna mpango wa kuvifufua vile vilivyokufa Mkoa kwa Mkoa.

Dkt.Jafo amesema hayo jijini hapa leo,Mei 15,2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio na mwelekeo wa Wizara hiyo katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Sita ambapo amesema mpango huo utahakikisha uwekezaji  huo unaleta mafanikio makubwa nchini.

“Katika mpango huo wa miaka sita ambao utaanza mwaka huu mwishoni mpaka mwaka 2031,miongoni mwa mambo yanayofanywa pamoja na ujenzi wa viwanda ni kuja na mikakati kuhakikisha viwanda vile vya zamani vinafufuliwa.

“Hesabu yetu ikienda vizuri ndani ya miaka hiyo sita tutakuwa tunafanya mambo mazuri hivyo nataka niwaombe wote waiopata viwanda fufueni vile viwanda kwa hiyari yenu kabla serikali haijaingiza mkono wake.

“Ili niombi langu kubwa sana kwenu wale ambao mmepewa viwanda ambao vingine vinaumiza,ukienda pale Tanga,Kiwanda cha mbao kipo karibu na Ofisi ya mkuu wa Mkoa kabisa,”amesema Dkt.Jafo.

Akizungumzia mafanikio ya Wizara hiyo Dkt.Jafo amesema kuwa Serikali kupitia Wizara hiyo imeendelea na jitihada za kukuza mauzo ya bidhaa nje ya nchi ambapo katika kipindi cha miaka minne mauzo katika soko la Jumuiya EAC yaliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 1,161.2 mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani milioni 1,163.8 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 0.22.
 
Huku Mauzo katika Soko la Jumuiya ya SADC yakiongezeka kutoka dola za Marekani milioni 1,303.4 mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani milioni 2,968 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 127.7.

Amesema kuwa Tanzania imekuwa na mwenendo mzuri wa mauzo katika nchi za bara la Afrika ambapo kwa mwaka 2024 mauzo yalikuwa dola za Marekani milioni 3,946.76 ikilinganishwa na dola za Marekani milioni 2,447.63 kwa mwaka 2021 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 61.2.

“Nchi imeendelea kunufaika na mpango wa AGOA ambapo mauzo kwenda Soko la Marekani kupitia mpango huo yameongezeka kutoka dola za Marekani milioni 33.06 mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani milioni 85.4 mwaka 2023 sawa na ongezeko la asilimia 158.3.

“Mauzo ya bidhaa katika soko la Nchi Wanachama wa Umoja wa Ulaya yameongezeka kutoka dola za Marekani milioni 891.5 kwa mwaka 2021 hadi kufikia dola za Marekani milioni 1,234.3 mwaka 2024 ikiwa ni ongezeko la asilimia 38.5,”amesema Dkt.Jafo.

Vilevile amesema kuwa Mchango wa Sekta ya Viwanda katika Pato la Taifa kwa mwaka 2024 ulikuwa asilimia 7.3 ikilinganishwa na asilimia 7.0 mwaka 2023. Aidha, ukuaji wa Sekta ya Viwanda ulikuwa asilimia 4.8 mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 4.3 mwaka 2023.

Kwa upande wa sekta ya biashara amesema mchango wa Pato  la Taifa kwa mwaka 2024 ulikuwa asilimia 8.6 ikilinganishwa na asilimia 8.4 mwaka 2023. Kasi ya ukuaji wa Sekta ya Biashara ilikuwa asilimia 4.8 mwaka 2024 ikilinganishwa na asilimia 4.2 mwaka 2023.