Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Dkt. Selemani Jafo ametoa muda wa siku kumi na nne kwa Uongozi kwa Wilaya ya Kinondoni kuhakikisha wanatatua tatizo la mfumo wa majitaka katika Mtaa wa Ufipa, Dar es Salaam.
Dkt. Jafo ametoa agizo hilo leo 25/02/2022 baaada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Mtaa wa Ufipa na kujionea uharibifu mkubwa wa mazingira utokanao na mfumo wa maji taka ambao miundombinu yake imeharibika na kutiririsha maji taka katika makazi ya watu.
Akiwa katika eneo hilo Dkt. Jafo amesikitishwa na maelezo ya wataalamu wa DUWASA, TARURA na Manispaa ya Kinondoni kutokuwa na habari ya changamoto inayowakabili wakazi wa eneo la Ufipa.
“Wataalamu msikae Ofisini tu, tokeni mje msikilize na kutatua kero za wananchi, haiwezekani mimi Waziri wa Mazingira nitoke Dodoma kuja kukagua na kuleta ufumbuzi wa tatizo hili wakati ninyi mpo hapa kila siku” Jafo alisisitiza.
Nae Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Bw. Godwin Gondwe amesema atahakikisha tatizo hilo linapatiwa ufufumbuzi ndani ya siku 14 kama Waziri Dkt. Selemani Jafo alivyoelekeza.
“Mhe. Waziri nikuhakikishie, sisi Wilaya ya Kinondoni kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi, siku ya Jumatatu yaani 28/02/2022 tutawasilisha kwako mpango kazi wa utekelezaji katika kutatua suala hili” Gondwe alifafanua.
Akizungumza kwa niaba ya wakazi wa eneo hilo Rajab Juma amesema changamoto hiyo ya majitaka katika makazi yao ni ya muda mrefu na imekuwa ni kero hususan kipindi cha mvua ambapo majitaka hufurika na kuhatarisha usalama wa maisha yao pamoja na kukabiliwa na mlipuko wa magonjwa.
More Stories
Mama Zainab:Watoto yatima ni jukumu la jamii yote
DC Korogwe awataka viongozi wa vijiji kuwatumikia wananchi kwa uadilifu
Premier Bet yamtangaza mshindi mkubwa