Na Daud Magesa, Timesmajira Online, Mwanza
MHADHIRI wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT), Dkt. Dotto Bulendu, amezungumzia changamoto inayoikabili jamii ya kulishwa habari hasi zaidi kuliko habari chanya ni kutokana na ujio wa mitandao ya kijamii.
Amesema kuna umuhimu kwa waandishi wa habari na viongozi wa dini kubadilisha mtindo wa uandishi wa habari, ili kusaidia kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii na kuepusha athari za habari hasi ambazo zinaathiri maadili ya vijana na jamii kwa ujumla.

Dkt.Bulendu,amesema hayo kwenye chakula kilichoandaliwa na BAKWATA Mkoa wa Mwanza, kwa ajili ya watoto yatima kutoka vituo 11 vilivyopo jijini humo,ambapo amehoji “Kwa nini watu wana chukiana, kwa nini nchi yetu imefika mahali mtu akifanya jambo jema wanaliacha na kutafuta mabaya,kwa nini mambo mema hayaendi.Upande wa dini mnayo majibu, sisi kwenye uandishi wa habari tuna majibu,”amesema Dkt.Bulendu na kuongeza:
“Tunasema ni ‘negativity’,tunawapa watu wetu vitu hasi hatuwafanyi wajitambue,kuthamini walicho nacho, kuipenda na kuithamini nchi yao.Mfano,mtu anaweza kuzungumza kwa saa 6 mambo mazuri asilimia 99, ikatafutwa asimilia moja mbaya ikawa habari,”.
Pia amesema,utoaji habari wa aina hiyo unasababisha watu kutopendana,kukata tamaa,msongo wa mawazo na sonona, ambapo habari kubwa zaidi zinazosumbua kwa sasa katika mitandao ya kijamii,ni za watu kuchukua uamuzi mgumu wa kukatisha uhai wao na kujiuliza kwa nini tumefika hapa.
“Ni kwa sababu ya habari tunazoilisha jamii zinawafanya wawe wakatili zaidi,watu kukata tamaa na kutokuipenda nchi yao,ipo haja ya kubadilisha aina habari na uandishi ili kujenga kizazi chema, tuwasaidie viongozi wa dini,isifike mahala wanatuletea watoto wenye maadili tunawaharibu kwa habari zetu tunazowalisha,”amesema.
Aidha amesema madhehebu ya dini yana vyombo vyao vya habari,hivyo watapeana elimu ya namna bora ya kutengeneza maudhui yanayotakiwa yatakayosaidia kujenga kizazi chema.
Amewasisitiza waandishi wa habari kama jamii,wanahitaji kubadilisha aina ya habari wanazozalisha ili kusaidia kujenga kizazi cha watu wenye maadili, huku akiwapongeza viongozi wa BAKAWATA kwa juhudi zao za kutunza watoto yatima.
Amekumbusha kuwa dini, kusaidia yatima ni jambo la msingi na kwa mujibu wa Mtume Muhammad S.A.W, kusaidia yatima ni sawa na kutekeleza ibada nyingine muhimu kama kufunga na kusali usiku,ameshauri waandishi wa habari kuwa sehemu ya mabadiliko hayo kwa kutoa habari zitakazosaidia kupambana na ukatili na maovu dhidi ya watoto, ikiwa ni pamoja na yatima.
Kwa mujibu wa Dk.Bulendu palipo na madrasa nyingi kuna uwekezaji mkubwa maana yake kuna kizazi chenye maadili,ambapo kutokana elimu nchini yanafanyika mapitio ya mitaala ili kutengeneza vijana wenye ujuzi zaidi waweze kumudu soko.

Awali Sheikh Hassan Kabeke amesema kuwa kila mwaka wanaandaa chakula kwa ajili ya yatima wakishirikiana na Mkurugenzi wa The Rocky Solution, Zakaria Nzuki,ambaye amekuwa akiunga mkono jitihada za Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,kwa kutoa mitungi ya gesi ya kupikia dhidi ya mapambano ya hewa ukaa .
“BAKWATA tunaongelea mustakabali wa nchi ,uchumi na maendeleo,tumeamua kuwa wazi ili kuondoa dhana ya upigaji ,tunajenga vituo vya afya ambapo Rais Samia ametuchangia sh. milioni 100, Naibu Waziri Mkuu, Doto Biteko sh.milioni Tano na Masanja Kadogosa, milioni kumi, hivyo bila amani, maji,barabara na umeme, havina maana na ndio sababu ya kuiombea nchi na Rais,”amesema.
More Stories
Dkt.Samia azindua jengo la Makao Makuu ya Mahakama,ataka kasi ya utoaji haki iendane na ubora wa jengo hilo
Dkt.Biteko :Mradi wa Kufua umeme wa JNHPP wakamilika rasmi
Msigwa :Wakuu wa mikoa andaeni maeneo ya upandaji miti