November 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Biteko:Umeme wa gridi ya taifa kuwaka Oktoba 2024,Katavi

Na George Mwigulu,Timesmajiraonline, Katavi.

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,Dkt. Dotto Biteko ameridhishwa na kasi ya ujenzi wa mradi wa umeme wa gridi ya taifa unaouganishwa kutoka Mkoa wa Tabora hadi Mkoa wa Katavi.

Wigo wa Mradi huo unahusisha ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme ya msongo wa kilovoti 132 wenye urefu wa Km 383 huku ukigharimu fedha Bilioni 116 na Bilioni 46.9 kwa ajili ya vituo vya kupozea umeme Inyonga na Mpanda huku wananchi wakilipwa fidia fedha Bilioni 5.378 kupisha mradi huo kwenye maeneo yao.

Dkt.Biteko akikagua ujenzi wa kituo cha kupozea umeme Mpanda leo,Julai 9,2024 licha ya kuridhishwa na ujenzi wa mradi huo amehimiza utendaji kazi kwa wakandarasi ili kuenda sambamba na mkataba.

“Tumekubaliana mwezi wa tisa lakini huu mwezi wa kumi nimewapa mimi kwenye mpango inatakiwa mwezi wa tisa mwishoni huu mradi uwe umekamilika lakini mimi nimewapa mwezi moja wa mwisho tunapokwenda kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa wakati tunaomba kura umeme uwe umewaka,amesema.

Naibu Waziri Mkuu huyo ameweka wazi kuwa serikali imedhamilia kuuingiza Mkoa wa Katavi kwenye historia tangu uhuru kwa mara ya kwanza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anaipeleka kwenye umeme wa gridi ya taifa.

“Tunaposema umeme wa Gridi ya Taifa maana yake umeme wa uhakika na kutoka kwenye majenereta ambayo yamechoka na ya muda mrefu,”amesisitiza.

Ameeleza kuwa mahitaji ya juu ya umeme katika mkoa huo ni Megawati 7 ambapo kimsingi wananchi kutokuwa huru zaidi kwenye matumizi ya umeme huo kwani mkoa unakasi kubwa ya maendeleo hususani kwenye uanzishwaji wa viwanda.

Serikali katika kutatua tatizo la umeme nchini Dkt.Biteko amebainisha serikali inampango wa kujenga mradi wa umeme kutoka Mkoa wa Iringa na kupitia mikoa ya Mbeya,Songwe,Rukwa na Katavi wenye uwezo wa kuzalisha kilovoti 400 na kukidhi zaidi mahitaji ya watumiaji.

Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Athanasi Nangali akisoma taarifa mbele ya Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Dotto Biteko amesema kuwa katika kituo cha kupokea na kupoza umeme Mpanda kilianza kujengwa mwenzi Septemba 2021 na sasa umekamilika kwa asilimia 97.

Ameeleza kituo cha kupozea umeme Mpanda kimeshafungwa transfoma yenye ukubwa wa MVA 35 sawa na megawati 28 ambapo fedha za ujenzi huo Bilioni 16.5 za ndani.

Aidha alibainisha kuwa ujenzi wa laini ya umeme wa msongo 132KV wa kutoka Tabora hadi Katavi kwa umbali wa Km 383 ambapo hadi sasa umefikia asilimia 63 huku matarajio yao hadi kufikia mwenzi wa kumi utakuwa umekamilika na huduma ya umeme wa gridi ya taifa kuanza kutumika.

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuamua kujenga historia ya kipekee mkoani humo kwani tangu uhuru haukuweza kufikiwa na umeme wa uhakika.

Mrindoko amesema kuwa mkoa huo hadi hivi sasa vijiji 172 vimefikiwa na umeme wa REA vilevile katika maeneo 114 tayari mkandarasi hupo kazini ili kuhakikisha maeneo ya pembezoni yanapoata umeme.

Ameeleza kuwa wananchi wanahamu kubwa wa kupatiwa umeme wa gridi ya taifa kutokana shughuri za kiuchumi na kijamii zinapata umeme ambao hautoshelezi.