September 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Biteko: Wizara ya Klimo,Mifugo kuweni karibu na wakulima,wafugaji

Na Esther Macha, Timesmajira Online, Mbeya

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt.Dotto Biteko ameziagiza Wizara za Kilimo na Mifugo kuwafikia wakulima na wafugaji kwa kutoa huduma za kitaalam ili kuweza kuzalisha mazao kwa tija ya kujiongezea kipato.

Dkt. Biteko amesema hayo Agosti 2,2024 wakati wa ufunguzi wa maonesho ya kilimo ya Wakulima Nanenane ambayo kikanda yanafanyika mkoani Mbeya katika viwanja vya John Mwakangale jijini hapa .

Ameeleza kuwa kilimo,mifugo na uvuvi ni eneo muhimu ambalo lazima serikali kuliangalia kwa ukaribu zaidi huku akiwahimiza wakulima na wafugaji wawatumie watalaam katika msimu wa maonesho ya Nanenane kujifunza na kuleta matokeo chanja ili mwaka ujao kuwe na sababu ya wakulima kuja tena kuongeza ujuzi.

Dkt.Biteko ameeleza kuwa kupitia mpango wa mbolea serikali itaendelea kuwezesha upatikanaji wake hapa nchini kwa wakulima kupitia ruzuku.

“Wakati natembelea mabanda nimeona hali iliyopo upande wa serikali kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya kuwapatia mbegu kupitia viwatilifu ili kufanya wakulima kuwa na kilimo chenye tija hivyo niwaombe wakulima na wafugaji kuendelea kuwatumia watalaam wenu mlionao katika kipindi hichi cha maonesho,amesema Dkt .Biteko.

Aidha Dkt.Biteko ameziomba taasisi za kifedha kuongeza kasi ya utoaji wa mikopo kwa wakulima na wafugaji huku akieleza kuwa kuna wakati masharti ya kupatikana kwa mikopo ni magumu kwa mkulima wa kawaida pamoja na kuhitajika vitu vingi.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Kilimo ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Tunduma,David Silinde amesema kuwa ukuaji wa sekta ya kilimo umeongozeka kutoka asimilia 2.7 wakati Rais Samia anaingia madarakani na kufikia 4.2 pamoja na utoshelevu wa chakula na usalama wa chakula nchini kuongozeka.

Amesema kuwa mauzo yanayotokana na kilimo awali ilikuwa Dola 1.2, lakini kwa sasa yameongezeka nakufikia Dola 2.3 ambayo ni ya zaidi trilion 7 za kitanzania.

Naye Meneja wa Benki ya Azania ambao wadhamini wakuu wa maonesho hayo ,Samson Mahimbi amesema wameamua kuwa wadhamini kwa sababu ya umuhimu wa sekta ya kilimo katika kuchangia pato la Taifa,kuongeza uchumi na kuwa chanzo cha ajira.