January 22, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko kufungua Maonesho ya Madini Geita

Na Mwandishi wetu, Timesmajira

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Dkt. Doto Biteko atazindua Maonesho ya Saba ya Kitaifa ya Teknolojia na Uwekezaji kwenye Sekta ya Madini Geita yaliyoanza Oktoba 2, kwenye viwanja vya Bombambili mkoani Geita.

Akizungumza katika Banda la Tume ya Madini Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Martine Shigella ambae aliongozana na Afisa Madini Mkazi wa Geita Mhandisi Samwel Shoo, amesema mwaka huu kuna washiriki zaidi ya 600.

Amesema, Maonesho ya mwaka huu yatakua na washiriki kutoka nchi mbalimbali ikiwemo Congo, Rwanda, Burundi na Kenya.

“Ni fursa kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa, watumie maonesho haya kuja kujifunza teknolojia mbali mbali zilizopo katika sekta ya madini, kuna Banda la Wizara ya Madini na Taasisi zake ikiwemo Tume ya Madini hivyo watanzania wenye nia ya kuwekeza kwenye sekta hii watembelee mabanda haya kujifunza na kupata elimu katika mnyororo mzima wa sekta ya madini,” amesema Mhe. Shigella.

Aidha, amewataka wachimbaji kujifunza Teknolojia ya utafiti wa madini katika hekari 120 na 130 na kwamba ukifanya utafiti lazima utumie teknolojia ya bei ya rahisi uweze kujua madini yanapatikana wapi na kwa kiasi gani.

Amesema pia watajifunza Teknolojia ya uchimbaji wa gharama nafuu ili mchimbaji asiingie gharama kubwa katika uchimbaji.

Pia watajifunza suala zima la uchenjuaji madini kutoka kwenye mawe, mchanga au udongo ikiwa ni pamoja na uongezaji thamani wa
dhahabu ili wananchi wapate dhahabu asilimia 90 ikiwa haijachanganywa hivyo ni fursa kwa wafanyabiashara kushiriki.

Wakati huo huo,Shigella amesema
Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ana dhamira ya dhati ya kuwathamini wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa na kwamba matunda yatokanayo na madini yananufaisha watanzania.

Amesema, miongoni mwa sheria zilizotungwa za asilimia 20 ya dhahabu kununuliwa na Benki Kuu, nia ni kuhakikisha Taifa linakua na akiba ya dhahabu ya kutosha.

“Mwaka jana kilo moja ya dhahabu iliuzwa kwa Dola 50,000 kwa sasa kilo moja inakwenda kwa Dola 70,000,” amesema Shigella na kuongeza

” Tungehifadhi dhahabu zetu tungekua na thamani kubwa kuliko kuhifadhi fedha za kigeni.” Amesisitiza

Shigella amewasihi wafanyabiashara waielewe Sheria hiyo, Benki Kuu imetoa taratibu za namna ya kununua dhahabu na kuondoa Tozo, bei iliyowekwa ni nzuri kuliko Dubai wanakopeleka.