December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Biteko kufungua maonesho ya Madini Geita

Na David John ,Timesmajira online Geita

NAIBU Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati Dkt.Doto Biteko anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika ufunguzi wa maonyesho ya Sita ya  Madini yanayofanyika mkoani Geita.

Akizungumza na waandishi wa habari katika viwanja vya EPZA vilivyopo katika Kata ya Bombambili mkoani humo Mkuu wa mkoa  Geita Martin shegela amesema kuwa maonyesho hayo yanatarajia kufunguliwa Septemba 23 mwaka huu  na washiriki mbalimbali kutoka nje na ndani ya nchi watashiriki maonyesho hayo.

 “ Maonyesho haya yalianza 2018 na mwaka huu ni maonyesho ya sita ya madini ambapo dhamira ni kuhakikisha kwamba wananchi wanapata maarifa mapya watakayoyatumia katika shughuli za utafiti,kuongeza thamani na shughuli za uchenjuaji,

“Mwaka jana tulikuwa na washiriki  250 ,lakini mwaka huu washiriki walioingia mpaka sasa ni zaidi ya 400 maana yake mwitikio ni mkubwa na wananchi hasa wachimbaji wameelewa maana ya uchimbaji hususani makampuni yanayojihusisha na uchimbaji,uchenjuaji ,uongezaji thamani kwa maana kwamba wameona umuhimu wa kushiriki katika maonyesho haya.”amesema Shigela

Pia amesema,Mkoa umeweka mazingira mazuri ili kuwawezesha wadau wa sekta ya madini kuja na teknlojia mpya na rahisi zitakazowawezesha wachimbaji wadogo kufaidika na teknolojia hizo kwa kuwa na gharama ndogo za uchjimbaji ,uchenjuaji na uongezaji thamani wa madini ili nchi ifikie hatua ya kuhifadhi dhahabu ambayo imeongezwa thamani kwa zaidi ya asilimia 100.

Mkuu wa Mkoa ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi hasa wanaojishughulisha na uchimbaji,uongezaji thamani na uchenjuaji wa madini kufika katika viwanja hivyo kujifunza na kujionesha mitambo na mshine kwa ajili ya shughuli za uchimbaji.