December 27, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Biteko asisitiza UVCCM kuwa chachu ya vijana wengine kujiunga CCM

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Zanzibar

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko leo  tarehe 8 Januari, 2024 amefungua Kongamano la  Umoja wa Vijana wa Chama cha Mapinduzi (UVCCM), Zanzibar ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya kuelekea miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Kongamano hilo ambalo limefanyika katika Wilaya ya Mjini, Mkoa wa Mjini Magharibi limeambatana na matembezi ya vijana nchi nzima kuhamasisha umuhimu wa Mapinduzi ya Zanzibar katika kuwaletea wananchi maendeleo.

Dkt. Biteko amesema kuwa, Jumuiya ya Umoja wa Vijana wa CCM ni silaha ya Chama katika uchaguzi na kupeleka maendeleo kwa wananchi na kwamba CCM inaona fahari na  heshima kubwa kuwa na vijana kama wao, “hata uchaguzi ukija tuna uhakika nguvu kubwa ya ushindi ipo, nawapongeza kwa kuweka rekodi na kuthibitisha kuwa mpo imara kwani rekodi hii bado haijawekwa na chama chochote kile.”

Kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo Zanzibar, amesema kuwa, kuna mabadiliko makubwa na miradi inayofunguliwa ni mingi na kwamba, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt. Hussein Mwinyi anafanya kazi kubwa kama ambavyo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan anaifanya katika kuwapelekea maendeleo wananchi hasa walio maskini ili kuinua hali zao za kiuchumi na kuweka miundo mbinu wezeshi ya kiuchumi.

Kutokana na juhudi hizo zinazofanywa na Viongozi Wakuu wa nchi katika kuwaletea wananchi maendeleo, ameitaka UVCCM kuhakikisha wanawasaidia viongozi hao katika kuyasemea mazuri wanayoyafanya tena bila kificho.

Katika utendaji kazi wa UVCCM, Dkt. Biteko ametoa angalizo kuwa, kwa sasa kuna wasomi wengi nchini na mitandao yenye kuunganisha watu wengi lakini suala hilo lisiwafanye waogope kutekeleza majukumu yao kwa kuwa watakosolewa kwani kukosea kupo katika safari ya mafanikio.

Amepongeza matembezi ya vijana hao yaliyofanyika nchi nzima kwani  wamekipa uhai Chama na kudhibitisha kuwa CCM iko imara kupitia UVCCM.

Kongamano hilo la kuadhimisha miaka 60 ya Mapinduzi ya Zanzibar limehudhuriwa na Mwenyekiti wa UVCCM Taifa, Komredi Mohamed Ally Kawaida, Naibu Katibu Mkuu, UVCCM, Mussa Haji Mussa, Makamu Mwenyekiti wa Chipukizi Taifa, Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Wajumbe Jumuiya ya Wazazi, Wenyeviti wa Mikoa wa UVCCM Tanzania, Makatibu wa Mikoa wa UVCCM, Wenyeviti na Makatibu wa UVCCM ngazi ya wilaya nchi nzima na Makatibu wa Hamasa.