*Aagiza Meneja Mkuu ETDCO kuondolewa
*Azitaka Taasisi za Wizara ya Nishati wasifanye kazi kwa mazoea
*Asema Watendaji wasioweza kuishi Maono ya Rais Samia wajitafakari
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko amekagua mradi wa ujenzi wa Kituo cha Kupoza umeme cha Uhuru kilichopo wilayani Urambo mkoani Tabora na kueleza kutoridhishwa kwake na kazi ya ujenzi wa laini ya msongo wa kV 132, kutoka Tabora hadi Urambo ambayo inatekelezwa na kampuni tanzu ya TANESCO (ETDCO).
Kazi ya ujenzi wa Kituo cha kupoza umeme cha Uhuru imegawanyika katika sehemu mbili ambapo ujenzi wa kituo cha kupoza umeme unafanywa na kampuni ya TBEA kutoka China, ambao wamefikia asilimia 84 ya utekelezaji huku kazi ya ujenzi wa laini ya umeme kutoka Tabora hadi Urambo (km 115), ikifanywa na kampuni ya ETDCO ambao wamefikia asilimia 10 tu ya utekelezaji.
Kufuatia hali ya kusuasua kwa ujenzi wa laini hiyo, Dkt. Biteko ameiagiza Bodi ya TANESCO kumwondoa Meneja Mkuu wa ETDCO Muhamed Abdallah ambaye ameonekana kutotoa kipaumbele katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati inayosimamiwa na Kampuni hiyo.
“Tarehe 17 Septemba, 2023 nilimtuma Naibu Waziri wa Nishati, Judith Kapinga kuja kukagua mradi huu ambaye aliwapa maelekezo ya kukamilisha mradi, pia nilimtuma aliyekuwa Mwenyekiti wa Bodi ya TANESCO, Meja Jenerali Paul Simuli kuja kukagua mradi huu 17 Desemba 2023 naye alitoa maelekezo ambayo hayajatekelezwa.
“Hatari iliyopo hapa ni kuwa TBEA atakamilisha kazi mapema mwezi Juni lakini umeme bado hautapatikana kwenye kituo kwa sababu laini ya umeme itakuwa haijakamilika.” Amesema Dkt. Biteko
Dkt. Biteko ameongeza kuwa, kutokukamilika kwa wakati kwa laini ya umeme kutoka Tabora hadi Urambo, kutapelekea Serikali kumlipa TBEA gharama ya kuwepo eneo la mradi bila kazi ambayo ni asilimia 0.2 ya gharama za mradi na hii ikiwa ni hasara kwa Serikali.
Amesema kuwa, kampuni ya TBEA na ETDCO zote zililipwa malipo ya awali ya utekelezaji wa kazi kwa asilimia 50 lakini ETDCO anatekeleza kazi kwa kusuasua huku TBEA akifanya kazi kwa wakati.
Kuhusu miradi ya umeme mkoani Tabora, Dkt. Biteko amesema kuwa, mkoa huo utaiunganisha mikoa miwili kwenye gridi ya Taifa kwani umeme kutoka mkoani humo utaenda pia Kigoma na Katavi kupitia kituo hicho cha Uhuru na baadaye kusafirishwa kwenda kituo cha kupoza umeme Nguruka na kwenda kituo cha Kidahwe mkoani Kigoma ili kuwaunganisha wananchi na gridi ya Taifa.
Ameongeza kuwa, Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan pia ametoa fedha kujenga laini ya umeme kutoka Tabora- Ipole-Mlele hadi Mpanda Mjini kwa urefu wa kilometa 393 na kwamba ujenzi wa kituo cha kupoza umeme Ipole umefikia asilimai 89, Mlele umefikia asilimia 87 na Mpanda Mjini umefikia asilimia 90 huku laini ya umeme ujenzi wake ukifikia asilimia 47.
Dkt.Biteko amesema nia ya Serikali ni kuwapa wananchi umeme na siyo maneno na ndiyo maana utekelezaji wa miradi mbalimbali inaendelea ikiwemo mradi wa Julius Nyerere ambao tayari mashine moja imeshaanza kuzalisha megawati 235 huku mashine nyingine ikikamilishwa mwezi huu ili kuingiza megawati 235 nyingine na hivyo kumaliza kabisa changamoto ya upungufu wa umeme.
Vilevile, Dkt. Biteko ameitaka kampuni ya ETDCO kujitathmini katika utekelezaji wa miradi yake kutokana na mingi kusuasua pamoja na kutathmini utendaji wake wa kazi ndani ya Menejimenti ambao si wa kuridhisha.
Vilevile, amewataka Watendaji wanaoona kwamba hawawezi kuishi na kutafsiri maono ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kujiondoa kwenye nafasi zao wenyewe ili kutorudisha nyuma juhudi za Serikali kutatua changamoto za Wananchi.
Kwa upande wake, Mbunge wa Urambo, Magreth Sitta amemshukuru Dkt. Biteko kwa kukagua mradi huo na kutoa maelekezo ambayo yatawezesha mradi huo kukamilika kwa wakati na kuondoa changamoto ya kukatika mara kwa mara ya umeme.
Aidha. Amemshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kupelekea fedha za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya umeme, maji, afya n.k katika Jimbo la Urambo.
More Stories
Zaidi ya wananchi 32,000 Vijiji vya Wilaya za Morogoro na Mvomero kuanza kupata mawasiliano
Wafanyabiashara waomba elimu ya namna watakavyorejea soko kuu
DCEA,Vyombo vya Ulinzi na Usalama vyafanya operesheni ya kihistoria