December 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Biteko amwakilisha Rais Samia Mkutano wa Kimataifa

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Namibia

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameshiriki katika Mkutano wa Kimataifa wa Hydrogen Barani Afrika unaoendelea Nchini Namibia akimwakilisha Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Mkutano huo unaohudhuriwa na washiriki zaidi ya 1000 kutoka ndani na nje ya Afrika, unajadili namna ya nchi za Afrika kushirikiana kuzalisha na kutumia Hydrogen kwa ajili ya kuzalisha umeme kwa Uchumi endelevu.

Akifungungua Mkutano huo Mjini Windhoek, Namibia, Makamu wa Rais wa Nchi hiyo, Netumbo Nandi-Ndaitwah amewataka washiriki kutumia fursa ya mkutano huo kuanisha mbinu na mkakati unaoweza kutumika kuleta maendeleo ya nchi husika kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Akitoa mfano wa Namibia, Makamu wa Rais alisema Namibia inajivunia matumizi ya Hydrogen kwa matumizi ya viwanda kwa manufaa nchi hiyo, nchi Jirani pamoja na mataifa mengine yaliyo katika mlengo wa matumizi ya nishati hiyo.

Aidha, amehimiza matumizi ya nishati safi kwa maendeleo ya nchi hizo huku akisisitiza ushirikishaji wa vijana kama nguzo muhimu ya maendeleo kwa bara la Afrika kutokana na mchango na uwezo wao kama nyenzo ya maendeleo katika nchi husika.

“Majadiliano haya ni muhimu yakazingatia ushirikishaji wa pande zote muhimu katika mkutano huu wa kimataifa ili kuwa na maendeleo ya kweli na endelevu kwa Uchumi na maendeleo ya watu nan chi zao” amesema Netumbo Nandi-Ndaitwah.

Awali katika majadiliano, Waziri wa Madini na Nishati wa Namibia, Tom Alweendo alisema wajumbe wa mkutano wanatakiwa kuzingatia kuwa nchi za Afrika na Washirika wake zinatakiwa kuzingatia kuwa matumizi ya rasilimali zilizopo yanahitaji ushirikiano badala ya ushindani.

Alisema Namibia imekuwa ikishirikiana na nchi nyingine barani Afrika katika matumizi rasilimali zilizopo na nchi nyingine washiriki zinakaribishwa kuunga mkono jitihada hizo ikiwemo uzalishaji na matumizi ya Hydrogen kwa ajili ya uzalishaji wa nishati safi ya kupikia.

Kwa upande wake, Waziri wa Nishati wa Ubelgiji, Tinne Van Der Straeten amewataka washiriki kuhimiza matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia ikiwa njia mojawapo ya kuwakomboa watu wan chi hizo dhidi ya umasikini.

Alisema matumizi ya nishati mbadala ikiwemo Hydrogen ni moja mkakati Madhubuti wa kuwakwamua watu na nchi zao katika lindi la umaskini na kuwawezesha kushiriki katika mipango mingine ya maendeleo.

Tanzanaia kwa upande wake, imetumia furasa ya mkutano huo kujifunza kuhusu faida na changamoto zinazoweza kujitokeza katika matumizi ya nishati safi kutokana na Hydrogen ikiwa ni pamoja na uzoefu kutoka nchi nyingine zinazotumia nishati hiyo.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko ameungana na Makamu wa Rais wa Namibia Netumbo Nandi-Ndaitwa kutembelea baadhi ya mabanda ya maonesho kuhusu matumizi ya Hydrogen yanayokwenda sambamba na Mkutano huo.

Baada ya maonesho hayo, Naibu Waziri Mkuu aliutana na Makamu wa Rais wa Namibia mazungumzo ya ndani na yaliyolenga katika mstakabali wa nchi hizo mbili.

Katika Mkutano huo, Naibu Waiziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Dkt. Doto Biteko amefuatana Balozi wa Tanzania nchini Namibia, Mhe. Cesar Waitara, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mha. Felchesmi Mramba na Kamishna wa Umeme na Nishati Jadidifu, Mha. Innocent Luoga.