February 11, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.bingwa wa watoto aikabidhi Hospitali ya Kanda Mbeya mashine mbili za kutoa dawa

Hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya yakabidhiwa mashine mbili na Daktari bingwa wa watoto

Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya

DAKTARI Bingwa wa watoto Dkt.Angela  Leonard amekabidhi Mashine mbili za kutoa dawa za mfumo wa kupumua kwa watoto wanaokabiliwa na magonjwa hayo(nebulizer mashines) kwa hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya ikiwa ni sehemu ya shukrani zake kwa hospitali hiyo pamoja na watumishi kwa ushirikiano waliompatia kipindi cha utekelezaji wa majukumu yake akiwa Katika hospitali hiyo .

Akikabidhi msaada huo kwa mkurugenzi mtendaji wa hospitali ya Rufaa kanda ya Mbeya leo Februari 11,2025 ameeleza kuwa wameamua kutoa msaada huo ili kuonyesha moyo wa shukrani kwa jamii aliyoishi nayo na kuihudumia vievile kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya afya nchini.

“Naamini kuwa, kila mtoto ana haki ya kupata matibabu bora,ninatumaini kuwa mashine hizi zitarahisisha mchakato wa matibabu na kuokoa maisha ya watoto wengi, pia nikiwa sehemu ya jamii naunga mkono jitihada za Serikali yangu katika juhudi za kusaidia upatikanaji wa huduma bora za afya ya mama na mtoto nchini.” Amesisitiza Dkt. Angela

Hata hivyo amesema kwamba eneo la watoto ni muhimu hivyo ndiyo Sababu ya kutoa mashine hizo mbili kwa hospitali yetu ya Rufaa kanda ya Mbeya ili kuhudumia watoto ambao wanakua ikiwa na mfumo wa kupumua.

Akizungumza wakati wa kupokea vifaa hivyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya Dkt. Godlove Mbwanji, amemshukuru Dkt. Angela kwa mchango huo mkubwa ambao utasaidia watoto wanaokabiliwa na magonjwa ya mfumo wa kupumua.

Dkt.Mbwanji amesema,“Mashine hizi ni muhimu sana katika hospitali yetu kwani zitatumika katika kutoa huduma bora za matibabu kwa Watoto hasa wanaosumbuliwa na magonjwa kama asthma, pneumonia na magonjwa mengine ya upumuaji.”

Aidha Dkt.Mbwanji, ametoa rai kwa jamii na taasisi mbalimbali kuwa na tabia ya kutoa sehemu ya shukrani zao za baraka ya mafanikio wanayoyapa kwa kupeleka misaada ya rasilimali fedha na vifaa tiba kwenye hospitali ili kusaidia wananchi,kwani jukumu la kuboresha upatikanaji wa huduma za afya nchini ni la kila mmoja wetu.

Hospitali ya Rufaa ya Kanda Mbeya inatoa huduma za matibabu kwa wakazi wa mikoa ya Nyanda za Juu Kusini, hivyo msaada huu ni hatua muhimu katika kuboresha huduma zinazotolewa.