February 13, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt.Batilda:Tumeanza mazungumzo waliotelekeza viwanda wanyang’anywe

Na Hadija Bagasha, Timesmajira Online, Tanga

MKUU wa Mkoa wa Tanga Balozi,Dkt.Batilda Burian,amesema wameanza mazungumzo na Hazina kuangalia uwezekano kwa waliopewa viwanda na kuvitelekeza kuwanyang’anya ili wapewe watu wenye uwezo wa kuviendeleza na sio kuacha magofu.

Balozi Batilda ameyasema hayo Februari 12,2025, wakati akizungumza na Viongozi wa dini na vyama vya siasa mkoani Tanga, ambapo amesema Mkoa huo umeanza mchakato wa kuvifufua viwanda vilivyokufa na hawataki kuona magofu.

Amesema,Tanga kulikuwa na viwanda vingi ambavyo vinafanya kazi ikiwemo kiwanda cha nondo,misumari,mbao na foma ambavyo watu walivichukua na kivitelekeza.

“Kwa Sasa tupo kwenye mazungumzo na hazina kuangalia uwezekano waliopewa hivyo viwanda wanyang’anywe na wapewe watu wengine,benki zipo, vijana wapo, BBT ya mama Samia jenga kesho iliobora ipo ambayo inawawezesha vijana waingie kwenye uwekezaji, mifugo,uvuvi, kilimo hata viwanda,”amesema Balozi Batilda.

Pia amewaomba viongozi wa dini kuhamasisha waumini kijitokeza kujiandikisha kwenye daftari la kudumu la wapiga kura ikiwemo kuboresha taarifa zao,ambapo zoezi hilo linaanza Februari 13 hadi 19,2025.