Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Waziri wa Ardhi,Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt.Angeline Mabula ameeleza kuwa serikali imetangaza msamaha kwa wadaiwa sugu wa ardhi kwa kulipa madeni yao bila riba katika kipindi cha Julai hadi Disemba 31 Mwaka huu.
Dkt.Angelina Mabula, amezungumza hayo wakati wa mafunzo ya uhamasishaji wa sensa ya watu na makazi kwa mwaka 2022 na mapambano dhidi ya ukatili kwa viongozi wa dini mbalimbali waliopo jimboni Ilemela kilichofanyika wilayani humo.
Ameeleza kuwa baada ya bajeti kupitishwa, kuna msahama mkubwa ambao Rais ameutoa kwa wale ambao wana madeni sugu ya muda mrefu ambapo taasisi zinazoongoza kwa kudaiwa madeni ya muda mrefu ni pamoja na taasisi za dini ambapo msahama huo unawahusu wadaiwa sugu kuanzia miaka mitano kurudi nyuma.
Pia ameeleza kuwa maendeleo ya nchi yanategemea sekta ya ardhi na isipo simamiwa vizuri basi changamoto hazitoisha,hivyo amewataka viongozi wa madhehebu ya dini kuhakikisha wanatumia fursa ya msamaha huo kulipa madeni yao.
“Niwaombe wote wenye madeni ya muda mrefu kutumia fursa hii kulipa madeni kwani pamoja na msamaha huo pia Rais Samia Suluhu Hassan ameridhia kupunguza tozo ya asilimia 1 ya kila mwezi ambapo hivi sasa italipwa kwa asilimia 0.5 katika kipindi hicho cha miezi sita na ifikapo mwezi Januari mwakani tozo hiyo itarudi kwenye kiwango chake cha awali,”ameeleza Dkt.Angeline.
Wakati huo huo Dkt.Angeline amewataka wenye maeneo ambayo yaliyochukuliwa kama ya umma lakini yanasoma majina ya watu binafisi kufanya marekebisho mara moja kwakuwa serikali haitakubaliana kuona migogoro inayotokea baina ya waumini na kiongozi wa dini wakilalamikia umiliki halali wa ardhi badala yake serikali itataka kuona viwanja kwa ajili ya kujenga nyumba za ibada viwe na majina ya wadhamini.
Akitolea ufafanuzi wa jambo hilo,Dkt. Angeline ameeleza kuwa dini ya kiislamu italazimika kusajili jina la Bakwata, halikadhalika madhehebu ya kikritu wataandika aidha TEC au wadhamini wengine kulingana na Imani zao.
“Tumekuwa na viwanja vingi ambavyo madhehebu yanagongana kwasababu tu jina la kiwanja linasomeka la mtu binafsi huku kikitambulika kama kiwanja cha dhehebu fulani, kama serikali hatukubaliani na jambo hilo,”ameeleza Dkt Angeline.
Pia ametumia fursa hiyo kuwataka viongozi hao kuendeleza maeneo ambayo waliomba kwa ajili ya kujenga nyumba za ibada pia kuyaweka katika utaratibu mzuri.
“Kuna viwanja ambavyo hamjaviendeleza ,angalieni maeneo yenu ambayo mmeomba kwa ajili ya nyumba za ibada yawe katika utaratibu mzuri na kuyaendeleza,”
More Stories
Madiwani Korogwe TC wahakikishiwa maji ya uhakika
CHADEMA wampongeza Mkurugenzi Mpanda
Ukosefu wa maji wasababisha wanafunzi kujisaidia vichakani