Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Askari wapya 256, wa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania(TAWA),wamehimizwa kuzingatia siri saba katika safari yao ya utumishi wa umma wa kulinda rasilimali za taifa ikiwemo maadili na kumtanguliza Mungu.
Hayo yameelezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii,Dkt.Hassan Abbasi,Februari 2,2026,wakati wa hafla ya kuhitimisha mafunzo ya kijeshi kwa askari wapya 256 wa TAWA, yaliofanyika katika Taasisi ya Taaluma ya Wanyamapori Pasiansi mkoani Mwanza.

Amesema,vijana hao leo wanaingia kwenye utumishi wa umma katika kipindi ambacho Dunia imejaa tashtutu na tashititi,hivyo amewataka wakazingatie mambo saba ikiwemo kuweka malengo,kuweka malengo makubwa,kujikita katika malengo,mawasiliano, nidhamu, uvumilivu na kutegemea Mungu katika safari yao ya mafanikio.
“Mambo saba ya kuzingatia  ni kuweka malengo,ya pili ni kuweka malengo makubwa kwa kiwango cha ‘Olympic’,ili ata ukifikia nusu hutakuwa hujapoteza,”amesema Dkt.Abbasi.
Amesema siri ya tatu ambayo wanapaswa askari hao kuzingatia ni kujikita(focus)katika kutekeleza na kuyaendea malengo yao.
“Jambo hili linatusisitiza kwenye kusimama kwenye ndoto na malengo yako,usipo sisimama utaenda kwenye ndoto za mwenzako hivyo utashindwa kufanya vizuri,”amesema Dkt.Abbasi.
Pia amesema siri ya nne ni mawasiliano ambapo kwenye utumishi wa umma kuna lugha zake ikiwemo lugha za heshima,staha ikianzia kati ya mfanyakazi na mfanyakazi, mfanyakazi na kiongozi pamoja na taasisi na taasisi.
“Tunapozungumzia mawasiliano ni pamoja na kuacha kiburi,lugha chafu matusi na lugha kali kwa wenzako kwani mawasiliano serikalini ni kitu muhimu,”amesema.
Huku akisisitiza kuwa siri ya tano ya kuzingatiwa ni maadili ili waweze kufanikiwa katika maisha yao huku akiwasisitiza kwenda kusimamia maadili binafsi na taratibu zilizowekwa katika kutimiza majukumu yao.
Huku akiwaonya wanapoenda kutekeleza majukumu yao ya kusimamia na kulinda rasilimali wajiepushe na vitendo vya rushwa kwani katika eneo ambalo watu wanaondoka katika jeshi la uhifadhi ni hilo ata kwa kujaribu kuchukua kitu kidogo.Â
“Mnakwenda kuanza kazi nchi ikiwa na tembo 60,000, waliopo maeneo mbalimbali nchini maana yake wakipungua tutaanza kuwalaumu nyinyi,Simba 17,000,nyati 225,000, chui 24,000,sheshe 4,447,hivyo nendeni mkazingatie maadili na kuepuka rushwa ambayo imewafanya wengi kuondolewa kazini,”amesema Dkt.Abbasi na kuongeza:
“Mkaishi kwenye njia mbalimbali za maadili kwani matendo yenu madogo yanaweza kuchafua Serikali na TAWA.Jambo la sita mkawe wavumilivu na siri ya saba mkaishi mkimtegemea Mungu,”.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ilemela,Amiri Mkalipa,amewahimiza askari hao wakafanye kazi kwa kuzingatia uzalendo, sheria, taratibu pamoja na kuepuka vitendo vya rushwa kwani wao ndio jicho,sikio,mkono na mguu wa Serikali.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya TAWA,Meja Jenerali Mstaafu,Hamis Semfuko,amesema watakaofanikiwa katika utumishi wao ni wale watakaozingatia nidhamu, uzalendo na uwajibikaji lakini wale ambao wataendekeza wizi,rushwa na kutokuwa na nidhamu wataishia njiani.



More Stories
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina
Kihongosi: Msigombane kwa itikadi za vyama