January 16, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dkt. Abbasi aimwagia sifa SBL udhamini Taifa Stars

a Mwandishi Wetu, TimesMajira Online

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Hassan Abbasi amesema kuwa, udhamini uliotolewa hivi karibuni kwa timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’na kampuni ya Bia ya Serengeti Breweries Limited (SBL) ni kielelezo cha namna ambavyo kampuni hiyo imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo ya michezo hapa nchini.

Mwanzoni mwa mwezi huu, kampuni ya SBL pamoja na Shirikisho la Soka Nchini (TFF) walisaini mkataba mpya wenye thamani ya Shilingi bilioni 3 baada ya kumalizika kwa mkataba wa awali ambao uliokuwa na thamani ya shilingi bilioni 2.1.

Ongezeko la kiasi hicho cha fedha za udhamini ulitokana na matokeo mazuri ambayo timu imekuwa ikiyapata katika kipindi cha miaka mitatu ya mkataba uliomalizika ikiwa ni pamoja na kufuzu kucheza Mashindano makubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika ikiwa ni baada ya miaka 39.

Akiipongeza kampuni hiyo kwa niaba ya Serikali, Dkt. Abbasi amesema kuwa, Serikali inatambua mchango unaoendelea kutolewa na kampuni hiyo kwani udhamini huo mkubwa ni kielelezo cha namna ambavyo kampuni hiyo ni mdau mkubwa kwa maendeleo ya michezo hapa nchini

“Mkataba ambao ulisainiwa kati ya SBL na TFF unaonyesha ni kwa kiasi gani kampuni ya Serengeti inathamini michezo na pia ni mdau mkubwa katika maendeleo ya michezo na hususani soka kwani kupitia udhamini uliopita tumeona nchi ikipiga hatua kubwa kwenye soka ikiwa ni pamoja na kuzalisha wachezaji wanaochezea Ligi kubwa za barani Ulaya kama Mbwana Samatta,” amesema Dkt. Abbasi.

Wakati wanasaini mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Mark Ocitti alisema, bia ya Serengeti Premium Lager ni mdau mkubwa wa michezo hapa nchini na kuongeza kuwa bia hiyo imekuwa ikijivunia kuwaunganisha Watanzania kupitia michezo.

“Kupitia bia yetu pendwa ya Serengeti Premium Lager, tunayo furaha kubwa kutangaza leo kutangaza udhamini kwa Timu yetu ya Taifa kwa kipindi kingine tena cha miaka mitatu. Tumechukua uamuzi huu kwa kuzingatia na kufahamu umuhimu wa michezo kwenye maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Tunaamini kwa kuidhamini Taifa Stars, siyo tu tunachangia katika maendeleo ya michezo bali pia tunachangia kukuza mpira wa miguu ambao watu wengi duniani na Tanzania wanaupenda sana,” amesema Mark na kuongeza.

“Tumeamua kusaini tena mkataba huu baada ya kuridhishwa na maendeleo pamoja na mafanikio ya timu kwa miaka mitatu iliyopita lakini pia kutoka na mapenzi makubwa ya Watanzania kwa timu ya Taifa,”.