January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dk Tulia aifuta machozi familia yenye mlemavu wa viungo Rungwe.

Na Esther Macha,Timesmajira Online,Rungwe

RAIS wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU),Mbunge wa Mbeya Mjini Dkt. Tulia Ackson ,ameifuta machozi familia ya Ambele Mwakipesile(36) mwenye ulemavu wa viungo kwa kujenga nyumba ya vyumba viwili na kuchangisha zaidi ya milioni 2.8 kwa ajili ya ujenzi wa chumba kimoja na matundu ya vyoo.

Hatua hiyo ya Dkt.Tulia kuishika mkono familia hiyo ni baada ya taasisi ya Tulia Trust kumuibua katika kijiji cha Kibatata Kata ya Kisondela Wilaya ya Rungwe kupitia mbio za kukimbiza bendera zilizofanyika kwa siku saba kuanzia Desemba 9 mwaka huu yenye ujumbe wa upendo,uwajibikaji na mshikamano.

Akizungumza na Wananchi wa kijijini hapo ,Dkt. Tulia ameonya wanaume ambao wanatelekeza familia ambazo wamezaliwa watoto wenye ulemavu.

Hata hivyo Dkt. Tulia amesema kuwa mbali na taasisi ya Tulia Trust ,kufanya tathimini na kujenga nyumba ya mhitaji huyo bado kuna changamoto ya miundombinu ya matundu na vyoo na chumba kimoja kwani vilivyojengwa ni viwili tu na yeye anaishi na mama yake mzazi.

Kauli hiyo ya Dk Tulia ilingwa mkono na wadau mbalimbali wakiwemo Watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Rungwe,akiwepo Mwenyekiti y wilaya ya Rungwe Mpokigwa Mwamkuga.

Akizungumza na wananchi kwenye mkutano wa hadhara ,Mwamkuga amesema wanakila sababu ya kumpongeza Spika ,Dkt. Tulia kwani amekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia miradi ya maendeleo na kuigusa jamii yenye uhitaji.

Naye Mbunge Vitimaalum Chama cha. Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Sophia Mwakagenda amesema kuwa uwepo wa Dkt.Tulia amesaidia vyama vya siasa kufanya maendeleo ya wananchi pasipo kujali itikadi za vyama.

“Tuendelee kumuombea Dk Tulia amekuwa ni kiongozi wa kujishusha kwa wananchi wa chini hata leo hii tunaona amefika kwa ajili ya kukabidhi nyumba za watu wenye ulemavu jambo ambalo linapaswa kumuunga mkono na kumuombea,”amesema.