September 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dk. Ndungulile akunwa sapoti ya Samia kinyang’anyiro WHO Kanda ya Afrika

*Ni pamoja na kuridhia , kumruhusu kuwania nafasi hiyo, aeleza mchuano mzima
ulivyokuwa hadi ushindi, ajiandaa kwenda Congo Brazzaville kuwatumikia Waafrika

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline, Dodoma

MKURUGENZI Mteule wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika, Dkt. Faustine Ndugulile amempongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia na kumruhusu kugombea nafasi hiyo na kwa jinsi alivyomsapoti katika safari hiyo nzima.

Dkt. Ndungulile alitoa pongezi hizo kwa Rais Samia na wengine waliomsadia kwenye kampeni za kuwania nafasi hiyo Bungeni jijini Dodoma wakati akitoa salamu za shukurani baada ya kukaribishwa na Naibu Spika wa Bunge, Mussa Zungu.

“Naomba kumpongeza Mheshimiwa Rais (Samia) kwa kuridhia kwake na kuniruhusu kugombea nafasi hii ya Mkurugenzi wa Shirika la Afya duniani kanda ya Afrika.

Lakini la pili kwa sapoti yake katika mchakato mzima katika safari hii. Kampeni hii Mheshimiwa Rais aliibeba, alikuwa ni ajenda yake ya kudumu pale alipokuwa anakutana na viongozi mbalimbali wa nchi pale alipokuwa anasafiri na wale waliokuwa wanakuja ndani ya nchi.,” alisema Dkt. Ndugulile na kuongeza;

“Kwa hiyo kwa njia ya kipekee kabisa napenda kumshukuru Mheshimiwa Rais.” alisema Dkt. Ndungulile. Alisema amepewa miezi sita kujipanga na kuandaa maono yake na atakapoanza kazi Machi, mwakani nia ya kufanya hivyo anayo, sababu za kufanya hivyo anazo na uwezo wa kufanya hivyo anao.

“Niwaombe mniombee, tuendeleze sala na dua nyingi kwani nafasi hii imebeba maono ya Watanzania na Waafrika wanatarajia makubwa, kikubwa niishukuru Serikali nzima na wabunge kwa kuniunga mkono.

Nitakuwepo katika kipindi cha mpito napokea maoni na ushauri kutoka kwenu,” alisema Dkt. Ndugulile ambaye amekuwa Mtanzania wa kwanza kushika nafasi hiyo na wa kwanza Afrika Mashariki.

Alisema amepewa kipindi cha miaka mitano kuonesha utendaji wake na iwapo atafanikiwa kufanya vizuri, anaweza kuchaguliwa tena kwa miaka mitano, hivyo kutumikia nafasi hiyo kwa vipindi viwili vya miaka mitano mitano, ambavyo ni sawa na miaka 10.

Kwa mujibu wa Dkt. Ndungulile kituo chake cha kazi kitakuwa Congo Brazzaville na kwamba kwa utaratibu ulivyo unapewa miezi sita ya kujipanga hivyo natarajia kuanza kazi mwishoni mwa Februari au Machi 2025.

“Wale waliokuwa wanahoji Jimbo la Kigamboni lipo wazi jibu ni hapana! Bado nipo nipo na wananchi wangu wote waliniunga mkono na walikuwa na dua zao pia.”

Akieleza alivyojinadi wakati wa kugombea alisema miongoni mwa mambo aliyogusia ni pamoja na namna Afrika inavyohitaji kuwa na uongozi imara na wenye maono kuhakikisha bara linaweza kufanikiwa, inahitaji mtu mwenye uwezo wa masuala ya kitaaluma, uongozi na sifa zingine.

Alisema katika nafasi hiyo alishindana na watu wabobevu, lakini anashukuru mawaziri wa afya waliona aina gani ya uongozi wanaouhitaji Afrika kwa sasa, hivyo walimchagua.

“Tunataka kuhakikisha huduma za afya zinapatikana barani Afrika, lakini kuona tunajiandaa vizuri na kuimarisha taasisi mbalimbali zinazofanyakazi katika Bara la Afrika katika uongozi wangu tunakwenda kuboresha WHO kuhakikkisha inakuwa imara.” Alisema.

Mbali na pongezi zake kwa Rais Samia, Dkt. Ndugulile aliwashukuru wabunge, spika na naibu spika na katibu wa Bunge kwa kumpa ushirikiano mkubwa wakati wote wa kampeni zake wa uchaguzi huo.

Alitoa shukrani zake kwa katibu na watumishi wa Bunge,akisema walimpa ushirikiano mkubwa ilibidi wakati mwingine asishiriki baadhi ya vikao vya Bunge.

Alishukuru akisema alipata meseji nyingi kabla na baada ya uchaguzi alienda na mawaziri wawili akiwamo Waziri wa Afya ambaye alikuwa na wiki tatu tu (Waziri wa Afya Jenista Mhagama) mawaziri wote, naibu mawaziri, makatibu wakuu wa wizara na wananchi wa Kigamboni kwa kunibeba.