November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Diwani wa Chadema amueleza Chongolo anavyotekeleza Ilani ya CCM

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Chemba.

DIWANI wa Kata Chandama kutoka Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Mohamed Mgongaji amueleza Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)Daniel Chongolo jinsi anavyotekeleza Ilani ya CCM katika miradi ya maendeleo.

Akizungumza katika mkutano wa shina namba moja la CCM,mbele ya katibu Mkuu huyo alipotembelea katika kata hiyo ikiwa ni muendelezo wa ziara yake katika majimbo yote ya Mkoa wa Dodoma yenye lengo la kukagua miradi ya maendeleo na utekelezaji wa Ilani ya CCM alisema kuwa yeye kama Diwani baada ya kuchaguliwa alishirikiana na miradi ambayo alikuwa anaisimamia na miradi hiyo ni kutokana na ilani ya chama cha mapinduzi.

“Kwasababu miradi iliyoko ni ya ilani ya chama cha mapinduzi na lazima nisimamie mimi kama diwani,nimesimamia miradi mingi ambayo imeshatekelezwa na imekamilika baadhi ya mradi ambao bado unasua sua ni mradi wa maji hiyo ndiyo changamoto kubwa mpaka sasa na hivi tunategemea katibu mkuu umekuja hili utalichukua angalau tuweze kuona hii changamoto hapa inaishije,”amesema Mgongaji.

Akijibu kuhusu suala la maji Chongolo alitoa siku saba kwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA)kupeleka umeme katika Kata hiyo ndani ya siku saba kwani ndiyo kikwazo kilicho tajwa na Wakala wa Maji Vijiji (RUWASA)kushindwa kuchimba visima kutokana na kutokuwepo kwa umeme utakaowezesha mitambo kuchimba kisima.

Hivyo amewaagiza RUWASA ndani ya muda wa wiki tatu wawewamefika mahala ambapo panatakiwa kuchimba kisima kwasababu umeme utakuwa umeshafika,wachimbe kisima ambacho wananchi watakitumia huku wao wakiwa wanaendelea kutengeneza mtandao wa maji ambao utasambazwa na sehemu zingine.