Na Judith Ferdinand, TimesMajira Online, Mwanza
Diwani wa Kata ya Nyamanoro wilayani Ilemela mkoani Mwanza George Maganiko,ameungana na wananchi wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki pamoja na kuunga jitihada zao katika kukarabati miundombinu ya barabara ya mtaa huo ili iweze kupitika na kuchochea maendeleo ya jamii.
Ambapo ameshirikiana na wananchi wa Mtaa huo katika ukarabati pamoja na kutoa vitu mbalimbali ikiwemo molamu(changarawe),mchanga,kokoto na mifuko ya saruji kwa ajili ya kumwaga zege katika baadhi ya maeneo ya barabara hiyo.
Akizungumza na timesmajira online wakati akishiriki ukarabati huo pamoja na wananchi wa Mtaa huo Maganiko amesema, barabara hiyo ni ya miaka mingi ambayo licha ya jitihada walizofanya awali bado inaonekana kuwa kizungumkuti ambapo wananchi kwa nafasi yao wamejaribu kukurabati.
Maganiko ameeleza kuwa kilichomsukuma kuunga mkono jitihada za wananchi ni baada ya kuona watu wanapata shida licha ya barabara zote zilizopo ndani ya Kata hiyo kuziombea fedha lakini bado hazijatoka.
“Katika kutembea kwangu kwenye ziara ya kukagua maeneo ya mitaa nilifika hapa nikaona hii barabara na nikaona na mimi napaswa kufanya jambo,nimetumia pesa zangu mwenyewe kununua molamu tripu 10,mchanga,kokoto na saruji tunapiga zege kuanzia huko chini mpaka huku juu na kipande kingine kilichobaki tunaweka molamu,”amesema Maganiko na kuongeza kuwa
“Nishukuru wananchi wa Nyamanoro Mashariki wameisha anza utaratibu wa kutengeneza barabara ambapo kila Jumamosi wanajitoa,hivyo niwapongeze kwa kufanya maendeleo na nitoe wito wajitokeze zaidi kwani maendeleo ni kwa ajili yao,”
Mwenyekiti wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki Zaituni Mlele,ameeleza kuwa baada ya kuona barabara hiyo imekuwa na changamoto aliwaita wananchi na kuanza zoezi la ukarabati ambao unafanyika kila Jumamosi.
Amemshukuru Diwani huyo kuwaunga mkono na kuungana na wananchi wa mtaa huo pia ameiomba serikali iweze kuwashika mkono ili barabara hiyo iweze kuwa imara na yenye kupitika vizuri.
“Tulikaa kikao na wananchi wakaridhia kuchangia kila kaya 1000, kwa ajili ya kutengeneza barabara imara kuanzia wiki iliyopita na leo Diwani ameweza kutuunga mkono baada ya kuona sisi wananchi wake tunahangaika sehemu ya kupita na tumepata shida sana hasa wajawazito tunawabeba mkononi badala ya kupita bajaji au gari,”amesema Zaituni.
Kwa upande wake Polisi Kata wa Kata ya Nyamanoro,Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Polisi Emmanuel Mwakalindile, amesema moja ya majukumu ni kuhamasisha maendeleo ya maeneo husika hivyo ukarabati wa barabara hiyo yeye pia anachangia kwa kuhakikisha inajengwa kwa kuhamasisha wananchi wa Nyamanoro Mashariki.
“Barabara hii itawezesha hata sisi Jeshi la Polisi kufanya doria maeneo haya kwa gari kwaio usalama wa maeneo haya yaendelee kuimarika kadri siku zinavyoenda kupitia falsafa ya Polisi jamii ni kuhakikisha ushiriki wa wananchi kwenye maendeleo ya Kata husika,ni na wajibu wa kukaa hapa kuhakikisha kila kitu kinaenda sawa,” amesema Mwakalindile.
Naye mmoja wa wananchi wa Mtaa wa Nyamanoro Mashariki Theresia Rogati, amewahimiza wananchi wote kushirikiana na Diwani kuweza kufanya ukarabati wa barabara zenye changamoto.
“Namshukuru Mungu kwa kazi yetu ya leo ineenda vyema kutokana na Diwani wetu kutuunga mkono katika kupambana na ukarabati wa barabara yetu,”amesema Theresia.
More Stories
Serikali kupeleka mawasiliano maeneo ya mipakaniÂ
Sekondari ya Butata mbioni kufunguliwa Musoma Vijijini
TIC yapongeza mradi wa Kampuni ya Big Best