December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Diwani Maanya ajivunia utekelezaji ilani kutokana na Uongozi madhubuti wa Rais Samia

Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online

DIWANI wa Kata ya Mbagala Kuu, Maanya Juma Maanya amesema amefanikiwa kutekeleza ilani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Kata hiyo kutokana na Uongozi madhubuti wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Pia amesema utekelezaji wa ilani hiyo umekwenda sambamba na maelekezo yaliyoelekezwa na Ilani ya CCM katika kipindi cha miaka mitano(2020/2025).

Maanya ameyasema hayo Jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki wakati akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa ilani ya CCM katika Kata hiyo kuanzia Octoba 2020 hadi Juni 2023 kwa wananchi na watendaji.

Amesema ushirikiano kutoka viongozi na watendaji wa serikali kuu, Serikali za mitaa na hamasa ya Wananchi wa Kata hiyo umemuwezesha kufanikiwa kuleta maendeleo katika kata hiyo.

Maanya amesema katika utekelezaji wa ilani hiyo amekuwa akisikiliza kero na malalamiko ya wananchi na kubaini kero zao kupitia kamati ya maendeleo ya kata kwa kukutana na viongozi wa CCM ngazi ya Kata na matawi.

“Nimetenga siku mbili kwa wiki kwa kuwepo Ofisi kwa siku ya Jumanne na Alhamisi ili kusikiliza na kushughulikia kero na malalamiko ya Wananchi, pia nimetenga siku maalumu katika wiki ili kuwasilisha kero mbalimbali za Wananchi kwa watendaji katika ngazi ya halmashauri ya manispaa ya Temeke,”amesema Maanya.

Akiitaja miradi ambayo amefanikiwa kuitekeleza ni miundombinu ya barabara, Afya, elimu, huduma ya maji safi na salama na usafi wa mazingira, maendeleo ya jamii, michezo ambavyo ni vipaumbele vya Wananchi katika Kata hiyo.

“Utekelezaji wa miradi hii mbalimbali ya maendeleo katika Kata ya Mbagala kuu kwa kipindi cha Octoba 2020 hadi Juni 2023 imefanikiwa kutokana na kushirikiana na kamati ya maendeleo ya Kata(WDC).

Amesema katika eneo la miundombinu ya barabara Kata ya Mbagala kuu kwa mujibu wa Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini TARURA Wilaya ya Temeke inao mtandao wa barabara wenye urefu wa kilometa 42.27 kati hizo Barabara za lami ni 14 sawa na kilomita 15.15, barabara za zege sawa na kilomita 1.25 na barabara bza chagarawe udogo 62 sawa kilomita 25.88.

Alibainisha miradi hiyo ya barabara imetekelezwa katika eneo la Jeshini kizuiani, kichemchem chalaina, kijichi Mbagala kuu Zakhem, Mbagala Sekondari,Kibaoni tawi la yanga, kichemchem maposeo .

Katika eneo la sekta ya Afya amesema utekelezaji umefanyika katika hospital ya Rangitatu Zakhem, Mbagala kuu zahanati ununuzi wa vifaa tiba, pamoja na upanuzi wa hospitali katika hospitali ya Rangitatu na Zakhem.

Kwa upande wa elimu amesema kuanzia Octoba 2020 hadi Juni 2023 kata ya Mbagala kuu imepokea jumla ya shillingi 776,800,000 kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya shule.

“Katika shule ya Mbagala kuu kumejengea madarasa 4, Mbagala kuu Sekondari madarasa 8, Mbagala Sekondari 2, Mbagala Sekondari matundu ya choo 20, Mbagala kuu shule ya msingi madarasa 5 na vyoo 3, kizuiani shule ya msingi ukarabati wa matundu ya vyoo 12.

Akizungumzia upande wa huduma ya maji safi na salama na usafi wa mazingira amesema kata hiyo imekuwa ikipata maji kupitia Mamlaka ya maji safi na usafi wa mazingira (DAWASA).

Amesema licha ya kupata maji kutoka DAWASA awajafikia hatua nzuri ya utoaji wa maji kwa wakazi wa kata hiyo kutokana na uhitaji wake kulingana na idadi ya watu kwa sasa.

“Kwa kutambua chagamoto ya maji katika Kata yetu kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo nimeweza kupata msaada wa visima viwili vya maji vyenye urefu wa mita 80 katika mtaa wa Jeshi la wokovu na mtaa wa kichemchem .

Awali Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Dar es salaam ,Abbas Mtemvu alimpongeza Diwani huyo kwa hatua ya kufanikiwa kuwasilisha ilani hiyo kwa wananchi.

Amesema Diwani huyo amefanya jambo njema hivyo aliwataka Madiwani wengine kuinga mfano huo na kusisitiza kuwa ni muhimu kila Diwani kutekeleza ilani ya CCM.

Diwani wa kata ya Mbagala kuu Maanya Juma Maanya akizungumza katika hafla hiyo ya kuwasilisha ilani ya kata hiyo kwa wananchi na watendaji.
Caption yakeDiwani kata ya Mbagala kuu Maanya Juma Maanya akimkabidhi ilani ya Chama Cha Mapinduzi CCM kata ya Mbagala kwa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Mkoa wa Dar es salaam Abbas Mtemvu