November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dirisha la huduma kwa wateja lafunguliwa kutoa taarifa zinazokiuka maadili shuleni

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online,Dodoma

KUFUATIA kuibuka kwa uwepo wa mafundisho na vitabu vyenye mafundisho kinyume na maadili ya kitanzania,Serikali kupitia Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia imefungua kituo cha huduma kwa wateja kwa ajili ya kutoa taarifa zinazokiuka miongozo na maadili katika taasisi za elimu.

Aidha amewasisitiza wamiliki wa shule kuhakikisha wanafuata Waraka Namba nne ambao unatoa muongozo katika shule zote nchini kuzingatia ubora wa elimu inayotolewa vinginevyo hatua kali zitachukuliwa kwa wahusika ikiwemo kufungia usajili wa shule husika.

Akizungumza leo Februari 3,2023 na waandishi wa habari Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt.Francis Michael amewaomba wananchi watoe taarifa kupitia simu ya mezani ya wizara hiyo yenye namba 0262160270  pamoja na simu ya mkononi namba 0737962965 .

“Kupitia kituo hiki tunawasihi wananchi watupe taarifa mbalimbali za ukiukwaji wa maadili katika taasisi zote za elimu kuanzia shule za msingi hadi vyuo lakini pia watupe taarifa zote zinazohusiana na masuala ya ukatili katika maeneo ya shule zetu ili  tuweze kuchukua hatua stahiki kwa wahusika kwa lengo la kumlinda na kumkinga mtoto”amesema Dkt.Michael

Aidha kuhusu vitabu vyenye mafundisho yaliyo kinyume na maadili Dkt.Francis alisema,Wizara ilitoa waraka namba 4 ambao unatoa muongozo katika shule zote nchini kuzingatia ubora wa elimu inayotolewa.

“Wizara katika kutekeleza wajibu wake kwa kusimamia utoaji wa elimu nchini na katika kuhakikisha kuwa njia mbalimbali za ufundishaji na ujifunzaji zinazingatia ubora,maslahi ya nchi,mila ,desturi na tamaduni za watanzania ilitoa waraka namba nne wa mwaka 2014 ambao pamoja na sheria na nyaraka nyingine na miongozo inayohusu elimu ulilenga katika kuhakikisha kuwa vitabu vya ziada na kiada vinavyotumika katika shule zote zilizosajiliwa nchini

“Vitabu vinatumika ni vyenye maudhui yanayoendana na mila ,desturi na utamaduni wa nchi yetu na kuweza kumlinda mtoto wa kitanzania aliyepo shuleni.”amesema na kuongeza kuwa

“Katika kusimamia utekelezaji wa waraka huu,wizara imebaini kuwa kuna baadhi ya shule ambazo zimekuwa zikiingiza na kutumia vitabu ambavyo maudhui yake yanakinzana na mila,desturi ,miongozo pamoja na tamaduni za kitanzania ambapo maudhui hayo yanahatarisha  ukuaji na malezi ya watoto na pia kupotosha mila na desturi za nchi yetu.”

Amesema vitabu hivyo visivyoruhusiwa orodha yake itatangazwa na Waziri wa Wizara hiyo Profresa Adolf Mkenda pamoja na kuweka zuio la matumizi ya vitabu hivyo.