March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DIB yawahikikishia wananchi usalama wa fedha zao


Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online, Tanga

BODI ya Bima ya Amana (DIB) imewahakikishia wananchi kuwa amana zao ziko salama, ikisema wateja wa benki zitakazofungwa au kufutiwa leseni na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) hulipwa fidia ndani ya kipindi cha mwezi mmoja baada ya tangazo rasmi kutolewa.


Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano wa Umma na Mawasiliano wa DIB, Lwaga Mwambande, alisema bodi hiyo inakinga amana za wananchi katika benki na taasisi za fedha zenye leseni ya Benki Kuu hadi kufikia Shilingi milioni 7.5 kwa kila mteja, hatua inayolenga kuimarisha imani ya wananchi katika sekta ya benki.

Alisema mteja yeyote mwenye amana isiyozidi kiwango hicho hulipwa fedha zake zote pindi benki aliyokuwa akiitumia inapofungwa au kufutiwa leseni na Benki Kuu.

Kwa wateja wenye amana zinazozidi Shilingi milioni 7.5, Mwambande alisema DIB, endapo imeteuliwa na Benki Kuu ya Tanzania kama mfilisi, huendesha mchakato wa ufilisi kwa kukusanya mali za benki iliyofutwa, kuuza na mapato yanayopatikana kugawa kwa waliokuwa wanaidai.


Akitoa mfano wa utekelezaji wa zoezi hilo, alisema wateja wa Benki ya FBME iliyofutiwa leseni mwaka 2017 wameendelea kunufaika na marejesho ya fedha zao, ambapo , katika awamu mbili zilizopita walilipwa jumla ya asilimia 55 ya madai yao, na Novemba 2025 yametangazwa malipo mengine ya asilimi 30, na hivyo kufanya wawe wamelipwa jumla ya asilimia 85 ya madai yao.


Aliongeza kuwa DIB inaendelea kusimamia mali za benki zilizofungwa ili kuhakikisha waliokuwa na amana wanapata marejesho makubwa zaidi kadri inavyowezekana.


Aidha, Mwambande alisema kuanzia mwaka jana, bodi hiyo imepanua majukumu yake kwa kuanza kuingilia kati mapema benki zinazoonesha dalili za kuyumba kifedha, kabla hazijafikia hatua ya kufilisika.


Kupitia ushirikiano na Benki Kuu ya Tanzania, alisema DIB inaweza kuruhusu utoaji wa mikopo au kuchukua hatua nyingine za kusaidia benki zenye changamoto kurejesha uthabiti wake na kuendelea kutoa huduma .