December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Diarra, Sopu kumaliza utata leo

Na Iddy Lugendo, Timesmajira Online

FAINALI ya kombe la Azam Sport Federation Cup imezidi kukonga nyoyo za mashabiki na wadau wa soka nje ya mchezo wenyewe macho ya wengi yanatamani kuona vita ya Mshambuliaji wa Azam FC Abdul Sopu na kipa wa Yanga Diarra.

Sopu ambaye kwa msimu uliopita aling’ara kwenye fainali ya Kombe la Azam Sport Federation Cup ilipowakutanisha Yanga na Coastal Union kwa kuweka rekodi ya mshambuliaji wa kwanza kumfunga kipa huyo mabao matatu kwenye mchezo mmoja, lakini pia alifanikiwa pia kumfunga mabao mawili kwenye ligi.

Huyu ndiye mshambuliaji ambaye amefanikiwa kumfunga Diarra mabao mengi kuanzia alipotua hapa nchini na wanakutana tena kwenye fainali mkoani Tanga.

Mshambuliaji huyo amesema nje ya maandalizi ya michezo ya Ligi lakini fainali hiyo ataibeba kwa uzito na kuandika historia nyingine akiwa na Azam.

Hii inakuwa fainali ya pili kwa Sopu kucheza dhidi ya Yanga baada ya ile ya msimu uliopita ambapo walivaana akiwa anaitumikia Coastal na wakalala kwa mabao 4-3.