March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dhana mpya kutoka Mfungwa hadi Mwanafunzi: Mageuzi makubwa Magereza

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online, Dodoma

KATIKA zama hizi za mabadiliko ya kiutendaji, Jeshi la Magereza limeamua kufungua ukurasa mpya unaolenga kuondoa dhana ya kale ya “mfungwa” na kuibua sura mpya ya “mwanafunzi gerezani”. Mabadiliko haya si tu ya kimtazamo, bali ni mkakati mahsusi wa kubadilisha maisha ya wafungwa kwa kuwapatia elimu, maarifa na ujuzi utakaowasaidia kujitegemea pindi watakapomaliza vifungo vyao na kuwa raia wema.

Akizungumza katika maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma Juni 19,2025 , Mrakibu Mwandamizi wa Jeshi la Magereza Elmas Mgimwa amesema kuwa Jeshi la Magereza sasa limejikita zaidi kwenye urekebishaji wa wafungwa kwa kutumia mbinu za kisasa za kielimu na kisaikolojia. “Tunataka jamii ielewe kuwa anayefika gerezani si adui wa jamii, bali ni mwanafunzi anayepitia hatua za marekebisho,” amesema.

Amesema ,katika kutekeleza azma hiyo, Jeshi la Magereza limeingia makubaliano na taasisi kama NACTVET ili kuandaa mitaala maalum ya ufundi kwa wanafunzi walioko gerezani. Kupitia makubaliano hayo, wafungwa huandikishwa rasmi kwenye kozi mbalimbali zikiwemo ujenzi, useremala, kilimo, na ufundi magari. Hii imewezesha baadhi ya wanafunzi kumaliza vifungo vyao wakiwa na stashahada halali zinazotambulika kitaifa.

Mbali na kuwaelimisha wafungwa, Jeshi la Magereza pia limejizatiti kubadilika kimuundo kwa kuunganisha mifumo ya kidigitali inayoboresha ajira, mishahara, na mawasiliano ya watumishi wake. Hatua hizi zimeongeza ufanisi na uwazi, na hivyo kulifanya jeshi hilo kuwa mfano bora wa mageuzi ya utendaji katika sekta ya umma.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Jeshi hilo, wafungwa wengi huingia gerezani wakiwa hawana taaluma yoyote. Hawa hupewa nafasi ya kujifunza stadi za maisha ambazo zitawasaidia kujitegemea wanaporejea uraiani. Wale wanaokuja na taaluma tayari, huendelea kubobea zaidi katika maeneo husika kupitia miradi ya karakana, kilimo na viwanda vidogo vidogo vilivyo ndani ya magereza.

Amos Shani ni mfano hai wa mafanikio ya mfumo huu mpya. Akiwa ameingia gerezani bila ujuzi wowote, sasa ni fundi maarufu wa kutengeneza makaro yasiyojaa. “Nina uwezo wa kupata kipato halali, nasomesha watoto wangu na pia nachangia pato la taifa,” anasema Amos, ambaye sasa yuko huru na anaendelea kuhudumia jamii kwa stadi alizopata gerezani.

Kwa muktadha huu, Jeshi la Magereza linatoa wito kwa jamii kuacha kuwatizama wafungwa kwa jicho la hukumu, bali kuwatazama kama watu wanaopitia mchakato wa kujifunza na kubadilika. Kwa kushirikiana, jamii inaweza kusaidia katika kupokea wahitimu hawa wa magereza kwa moyo wa matumaini na usaidizi, badala ya unyanyapaa.

Kwa ujumla, mageuzi haya ya kutoka mfungwa hadi mwanafunzi ni hatua madhubuti ya kulijenga taifa lenye misingi ya haki, elimu na usawa. Ni mwaliko kwa kila mmoja wetu kutambua kuwa mabadiliko ya kweli huanza na mtazamo mpya – mtazamo unaoona gerezani kama darasa la pili la maisha, si gereza la mwisho la matumaini.