November 5, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Dhamira ya Samia uimarshaji huduma za afya yatua Kata Bwawani, TASAF yamaliza kilio cha wananchi

Na Reuben Kagaruki,Timesmajiraonline,Arusha

ILI kufikia azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Watanzania wanakuwa na afya bora, Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) umeendelea kufanyakazi kubwa ya ujenzi wa miundombinu ikiwemo vituo vya afya kupitia fedha za OPEC hadi maeneo ya pembezoni mwa nchi.

TASAF imeendelea kutekeleza kwa vitendo dhamira ya Rais Samia ya kuboresha afya za wananchi wote ili kuwa na jamii yenye afya bora na Ustawi, ambayo itachangia
kikamilifu katika maendeleo ya mtu binafsi na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Uthibitisho wa haya ni ujenzi wa Kituo cha Afya kilichojengwa katika Kata ya Bwawani yenye vijiji vinne katika Halmashauri ya Arusha DC, ambapo katika Kijiji cha Themi ya Simba, ndiko TASAF imejenga kituo cha afya kwa gharama ya sh. milioni 600, huku wananchi wakichangia asilimia 10 ya nguvu kazi.

Ujenzi wa kituo hicho utaokoa maisha ya wakazi wa Kata Bwawani, ambao walikuwa wakilazimika kutembea umbali wa kilometa zaidi ya 10 ha 50 kufuata huduma za afya.

Ujenzi wa kituo hicho unakwenda kupunguza kama sio kuhitimisha vifo vya wananchi wengi vilivyotokana na kukosa huduma karibu karibu ambapo wanawake wajawazito waliokuwa wakipakizwa kwenye tela zinazokokotwa na punda kupelekwa kwenda kupatiwa matipababu kituo cha Afya cha Nduruma.

Mkurugenzi wa Mkuu wa TASAF, Shederack Mzaray, anasema wananchi wa kijiji hicho, walitambua kwamba wanakabiliwa na changamoto ya kupata huduma za afya, kwani kutoka kijijini hapo hadi eneo ambalo huduma za afya zinapatikana ni zaidi ya kilometa 10.

Anasema wananchi waliibua mradi huo na kupitia TASAF na Halmashauri ya Arusha, walianza kuutekeleza mradi huo. Kwa mujibu wa Mziray hadi sasa kwenye ujenzi wa Kituo cha Afya Bwawani kuna majengo manne.

Mziray anataja majengo hayo kuwa ni jengo la Wagonjwa wa Nje (OPD) maabara kubwa, eneo la kujifugulia wazazi, jengo la kupumzikia na nyumba za kukaa watumishi za familia tatu (Three in One) ambapo ujenzi wote huo umegharimu zaidi ya sh. milioni 600 pamoja na nguvu za wananchi.

“Kawaida miradi hii inashirikisha jamii, ambapo inatakiwa ichangie asilimia 10 ya gharama za mradi.

Maofisa wa TASAF pamoja na waandishi wa habari wakiangalia miundombinu iliyojengwa kwenye Kituo cha Afya cha Bwawani, kilichopo Halmashauri ya Arusha DC.

Napenda kuwapongeza wananchi wa hapa na Serikali ya Rais Samia kwa kazi kubwa ambayo imefanyika hapa kwa kweli, ni mbali sana kutoka makao makuu ya Halmashauri, lakini wananchi wamefanyakazi kubwa kwenye mradi huu ambao tuna uhakika utaenda kutatua kero ya wananchi wa maeneo hayo.

Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF Halmashauri ya Wilaya Arusha DC, Sulemani Msumi, anasema Kata ya Bwawani ni moja ya kata zilizopo pembezoni Arusha DC. Anasema kutokana na sababu ya umbali, wananchi waliibua mradi huo wa huduma za kiafya, kwani wananchi walikuwa wakipata huduma za afya Nduruma.

Anasema ilipokuwa ikitokea mgonjwa wakati wa changamoto ya mafuriko huduma za afya zinakuwa shida, kwani inakuwa vigumu wananchi kufika Kata ya Nduruma ambako wana kituo cha afya, ndiyo maana waliamua kuanzisha mradi huo.

Anasema kituo hicho kinakamilika mwaka huu na kitahudumia watu zaidi ya 20,000 , hasa kwa kuzingatia kwamba Kata ya Bwawani inapakana na Wilaya ya Simanjiro upande wa Magharibi, hivyo wananchi wa wilaya hiyo watakuwa wakipata huduma kituoni hapo.

Aidha, Msumi anasema Kata ya Bwawani ina vijiji vinne, Kijiji cha Themia Simba, Nyamgusi, Kigongoni na Bwawani.

” Vijiji vyote hivyo vinatarajia kupata huduma hapa, pamoja na zahanati tulizo nazo, lakini hazikidhi huduma mbalimbali kama vile upasuaji ambazo tunatarajia kuanza kuzipata hapa (Bwawani),” anasema.

Anasema kwenye kituo hicho tayari wamejenga majengo manne ambayo ni pamoja na jengo la wagonjwa wa nje ambalo litakuwa linafanya shughuli nyingi kwa wakati mmoja, kwani kuna vyumba vya sindano, vidonda, ofisi za madaktari na sehemu ya kutolea dawa.

Mwonekano wa majengo

Anasema jengo hilo la wagonjwa wa nje limegharimu sh. milioni 117 hadi ukamilishaji wake. Kwa mujibu wa DED jengo lingine ni la maabara ambalo hadi kukamilika kwake limegharimu sh. milionin 95, ambapo wanatarajia kuwa na vifaa tiba na vipimo vya kisasa kwa ajili ya wananchi kupata vipimo vya uhakika.

Aidha, anasema kuna jengo kwa ajili ya kujifungulia ambalo lina sehemu ya kujifungulia, mapumziko baada ya akina mama kujifungua na lenyewe lipo kwenye hatua ya kukamilika. “Lakini pia tuna nyumba kwa ajili ya Watumishi (Three ni one) ambapo kila moja ina vyumba vitatu, chumba kimoja Master bed room na vyumba viwili vya kawaida.

Aidha, nyumba hizo zina jiko, sebule na zote ziko kwenye mfumo mmoja na zimegharimu sh. milioni 101 katika ukamilishaji wake,” anasema na kuongeza; “Ujenzi wa kituo hiki kupitia mradi wa TASAF unaenda kubadilisha historia ya wananchi wa Bwawani na wananchi wa Arusha kupitia Halmashauri Arusha DC.

Kwani kama tunavyofahamu hii ni kata ambayo ipo pembezoni kulikuwa na vifo vingi kwa watoto na akina mama kwa kufuata huduma za afya mbali. Kwa hiyo tunashukuru uongozi wa nchi yetu kupitia kwa Rais Samia kwa kuwiwa na kuleta fedha hizi kupitia OPEC.”

Mwonekano wa majengo katika hatua mbalimbali

Naye Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Themi ya Simba, Fredy Kassale, anampongeza Rais Samia kwa kuwezesha TASAF kuwajengea kituo hicho cha afya.

Kassale anasema kutokana na changamoto waliyokuwa wakikabiliana nayo ya kukosa huduma za afya karibu , wananchi walihamasika wakakusanya mawe zaidi ya lori 19 na tofari 4,000.

” Kwa hiyo viongozi walipofika wakakuta wananchi wamesomba mawe na matofari na kuyarundika kwenye kiwanja hiki wakaona kabisa kwamba wana uhitaji wa huduma za afya karibu,” anasema Kassale.

Kwa mujibu wa Kassale baada ya hapo waliitisha mkutano wa Kijiji wakaandika mhutasari na maombi wakiomba TASAF iwasaidie kujenga kituo cha afya. Anasema maombi hayo waliyapeleka kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Arusha DC walikubaliwa.

“Ndipo tulipopatiwa fedha za TASAF, wananchi waliendelea kujitolea nguvu kazi zao kwa kuchimba misingi yote ya majengo mnayoyaona hapa , kukoroga zege na zote hizo walizifanya kwa kujitolea,” anasema.

Mandhari ya majengo

Anasema kazi hiyo ilifanywa na wanakijiji wote, vijana, wanaume na wanawake na kwamba mwitikio ulikuwa mkubwa.

“Wananchi walikuwa na uchungu kwa sababu wanawake wengine walikuwa wanabebwa kwa tela linalokokotwa na punda kupelekwa hospitali Nduruma, wengine walikuwa wakijifungulia njiani na wakati mwingine mama akawa sio riziki, walipopata adha hiyo, ndipo wakapambana kwa hali na mali kuhakikisha wanapata kituo cha afya na ndiyo hatua hii tuliyofikia.

Na sisi kama viongozi tuliwasimamia, tukawatia moyo na fedha zilipoletwa tulifanyakazi pamoja hadi hatua hii tuliyofikia ndiyo maana tunapongeza Serikali ya Mama Samia kwa hatua hii,” anasema.

Aidha, anasema kituo hicho kitakuwa mkombozi kwani Kata ya Bwawani ikabiliwa na tatizo la maji linalochangia magonjwa ya matumbo na watu kutapika damu.

Diwani wa Kata ya Bwawani, Justine Siray, anasema wamefarijishwa sana na ujenzi wakituo hicho cha afya kwani kikamilika kitakuwa na uwezo wa kuhudumia watu 20,000 na wao watakuwa wanufaika wakubwa, kwa sababu walikuwa mbali mno na vituo vyote vya afya.

“Mfano kutoka hapa hadi uende Kituo cha Afya Nduruma ni karibia kilometa 25 na kutoka hapa hadi Arusha Mjini ni karibia kilometa 55, kwa hiyo akina mama walikuwa wanpata adha kubwa wakati wa ujauzito na wakati wa kujifungua.

Kwa sababu usafiri wenyewe na barabara siyo rafiki kwa hiyo wakati mwingine mnaweza kujaribu kumbeba mjamzito kwenye toyo wakati mwingine anazidiwa njiani na hata kupoteza maisha yeye na mtoto,” anasema Siray.

Kutokana na ujenzi wa kituo hicho kupitia TASAF, diwani Siray anamshukuru Rais Samia na wasaidizi wake kwenye halmashauri , kwani wamenufaika kwa ujenzi wa kituo hicho, hali haikuwa sio shwari kwa wananchi wanaowaongoza.

Anasema kwa ujenzi wa kituo hicho, afya za wananchi zitaimarika, mama na mtoto wataenda kuwa salama, wanaamini hivyo kwa sababu kwa kipindi cha nyuma hali ilikuwa mbaya.

Kwa sasa anasema wanatamani kupata jengo mochwari, wodi ya wanawake, wanaume na jengo la utawala pamoja na kichomeataka.

“Kwa hiyo tunavyohitaji ni ni hivyo, lakini tunaamini kilichofanyika hadi sasa ni kikubwa kuliko hivyo na kwa kuwa Serikali chini ya uongozi wa Rais Samia kwa niaba ya wananchi wetu inawezekana akatutazama tena kwa jicho la huruma ili na sisi tuliopo pombezoni tuweze kuonekana na tusijione hatuonekani.

Kwa hiyo kwa niaba ya wananchi wangu wa Kata ya Bwawani na kwa niaba ya TASAF mfikisheni Rais Samia salamu zetu, kwani tutakuwa wanufaika wakubwa wa kituo hiki cha afya,” anasema Diwani Siray.