
Na Esther Macha , Timesmajira Online Mbeya
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbeya imempongeza Mh. Aida Haule, Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo na Diwani wa Kata ya Utengule Usongwe, kwa ushindi aliopata na kuchaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti wa ALAT Mkoa wa Mbeya.
Katika uchaguzi huo uliofanyika Januari 27, 2026 kulishindanishwa wagombea wawili: Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Kelvin Shishi, na Mh. Aida Haule ambaye aliibuka mshindi.
Akizungumza na waandishi wa Habari, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Bi. Erica Yegella, amesema uongozi wa halmashauri unampongeza Mh. Aida kwa ushindi huo ambao, amesema, utaendelea kuisaidia Halmashauri hiyo kusonga mbele katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Kwakweli sisi kama Halmashauri tunampongeza sana Mh. Aida. Ushindi wake ni faraja kubwa na tunamtakia heri katika majukumu haya mapya. ALAT ni chombo muhimu kinachosaidia serikali za mitaa katika usimamizi wa fedha, miradi na maendeleo ya wananchi. Tunajivunia kuwa na Mwenyekiti mahili kama Mh. Aida,” amesema DED Yegella.
Ameongeza kuwa Halmashauri ina miradi na majukumu katika sekta mtambuka kama maji, afya na elimu, hivyo uwepo wa kiongozi kama Haule ni jambo la kujivunia.
“Mimi najivunia kuwa na Mwenyekiti msomi mwenye shahada, na katika Mkoa wa Mbeya ndiye Mwenyekiti pekee mwanamke miongoni mwa Halmashauri saba. Kugombea na kushinda kwa kishindo ni heshima kubwa. Mimi kama katibu wake nitaendelea kuwa mwadilifu na mwenye nidhamu, kwa sababu ninayaona anayofanya—ni makubwa,” amesema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti mpya wa ALAT Mkoa wa Mbeya, Mh. Aida Haule, amesema atatumia nafasi hiyo kuimarisha mshikamano na ushirikiano baina ya madiwani wa Halmashauri zote saba za Mkoa wa Mbeya ili kuleta matokeo chanya kwa wananchi.
“Hiki ni chombo muhimu sana katika kuwasilisha taarifa na mahitaji ya Halmashauri kuanzia ngazi ya wilaya, mkoa hadi taifa. Nimeichukulia nafasi hii kwa uzito mkubwa. Naahidi kutoa ushirikiano kwa madiwani wote na kushirikiana na Mwenyekiti wetu wa ALAT Mkoa, Mh. Dour Mohamed, ambaye ni Meya wa Jiji la Mbeya,” amesema Haule.
Elizabeth John, mkazi wa Mbalizi, amesema ushindi wa Mh. Aida ni heshima kubwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya na kwa wanawake wa mkoa huo.
“Tutamlinda kwa gharama yoyote kiongozi wetu. Ametuheshimisha sisi wanawake. Katika mkoa wenye Halmashauri saba, kuwa na Mwenyekiti pekee mwanamke ni hatua kubwa, halafu leo anakuwa Makamu Mwenyekiti wa ALAT Mkoa—ni fahari. Tuna Mkurugenzi mwanamke ambaye ni mfuatiliaji na mtendaji mzuri, hivyo tunaamini Halmashauri yetu inasonga mbele,” amesema.

More Stories
Kihongosi amtaka mkandarasi kuwalipa vibarua stahiki zao
DC Mbozi afuturisha wananchi, asisitiza mshikamano na Umoja.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali: Nina imani mubna utendaji kazi wa ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria