Na Moses Ng’wat, Timesmajira Online,Tunduma.
HALMASHAURI ya Mji wa Tunduma, Wilaya ya Momba, mkoani Songwe ipo kwenye mchakato wa kufanya upanuzi wa Maegesho (Truck’s Parking) ya magari makubwa yanayovuka mpaka wa Tanzania na Zambia, kutoka malori 120 hadi malori 300 kwa lengo la kusisimua na kuiongezea Halmashauri hiyo mapato yake ya ndani.
Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Philemon Magesa, katika mahojiano maalum na Timesmajira Online yaliyolenga kupata taarifa zinazohusiana na utekelezaji wa mikakati ya ukusanyaji wa mapato ya ndani na kusababisha mapato hayo kuongezeka mara dufu.
Halmashauri ya Mji Tunduma imeongeza wigo wa ukusanyaji wa mapato ya ndani kutoka katika vyanzo vyake mbalimbali, ikiwemo miradi ya kimkakati na kufikia kiasi cha shilingi bilioni 13.7 kwa mwaka.
Akifafanua zaidi kuhusu utekelezaji wa mradi huo wa upanuzi wa maegesho ya magari makubwa yanayovuka Mpaka wa Tanzania na Zambia (Truck’s Parking), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Magesa alisema utaongeza ukusanyaji wa mapato ndani kutoka shilingi milioni 100 hadi kufikia shilingi milioni 300 kwa mwaka katika chanzo hicho.
“Manufaa ya kutanuliwa kwa mradi huu wa Maegesho kutoka magari makubwa 120 hadi 300 yanayovuka Mpaka wa Tanzania na Zambia (Truck’s Parking) ukikamilika unatarajia kuiongezea Halmashauri hii mapato kutoka mapato ya awali ya shilingi milioni 100 kwa mwaka hadi kufikia Shilingi milioni 300”.
“Halmashauri hii ina vipaumbele mbalimbali katika utekelezaji wa shughuli zake za kila siku na kipaumbele namba moja kabisa ni ukusanyaji wa mapato na miongoni mwa fedha zinazokusanywa zinapelekwa kutekeleza miradi mingine ya kimkakati kama huu wa maegesho kwa lengo la kusisimua makusanyo ya mapato ya ndani”.
Aidha, Mkurugenzi Mtendaji Magesa amesema katika utanuzi huo kutakuwepo mradi wa ujenzi wa Mgahawa wa chakula (Reustaurant), pamoja na nyumba za kupumzika madereva na wasaidizi wao (Rest house).
Katika hatua nyingine, Magesa alieleza namna Halmashauri hiyo inavyoendelea kunufaika na miradi ya kimkakati iliyojengwa katika Halmashauri hiyo, ikiwemo ule wa kituo cha Kikuu cha mabasi Mpemba.
Amesema kituo hicho kilichojengwa kwa zaidi shilingi bilioni 1.6 fedha kutoka serikali kuu kimesaidia kuongeza wigo wa makusanyo ya ndani.
Amesema awali kabla ya kujengwa kwa kituo hicho Kikuu cha mabasi yaendayo mikoani, Halmashauri hiyo ilikuwa ikipata kiasi cha shilingi milioni 150, lakini baada ya ujenzi kukamilika sasa Halmashauri hiyo inakusanya jumla ya shilingi milioni 260 kwa mwaka.
More Stories
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu
Airtel yatoa zawadi kwa wateja wake
Mpango ashiriki mazishi ya Mama yake Serukamba