Na Esther Macha,TimesmajiraOnline, Mbarali
HALMASHAURI ya Wilaya ya Mbarali mkoani Mbeya imeanza utekelezaji wa mkakati maalumu wa kuhakikisha shule zote shikizi zilizopo wilayani humo zinatambuliwa rasmi kisheria, ikiwemo kusajiliwa kwa mujibu wa taratibu za Serikali.
Akizungumza na Timesmajira Desemba 12, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbarali, Raymond Mweli, amesema tayari ametoa maelekezo katika vikao mbalimbali kwa wataalamu wa elimu kuhakiki na kubaini shule zote shikizi ili zipate utambuzi rasmi.
Amesema shule shikizi 20 zilizopo wilayani Mbarali zitahakikiwa ili kubaini vijiji, kata na tarafa zinakopatikana, hatua itakayowezesha kupata takwimu sahihi za wanafunzi na kuboresha upangaji wa rasilimali, huku lengo kuu likiwa ni kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi.
“Utambuzi wa shule hizi utatuwezesha kujua idadi ya wanafunzi waliopo na kupanga mipango sahihi ya elimu, ikiwa ni pamoja na kusogeza huduma karibu zaidi na watoto wetu,” amesema Mweli.
Ameongeza kuwa Halmashauri pia imejipanga kupeleka walimu wa kutosha katika shule hizo shikizi ili kuondoa changamoto ya upungufu wa walimu na kuhakikisha ufundishaji unakuwa na tija.
Kwa upande mwingine, Mweli amesema utekelezaji wa mkakati huo utazingatia upatikanaji wa bajeti na ushirikiano na wadau wa maendeleo, akisisitiza kuwa Halmashauri ya Mbarali ina uhusiano mzuri na wadau mbalimbali wanaosaidia shughuli za maendeleo.
Amesema pia Halmashauri inapanga kukutana na wadau ili kushirikiana katika kupunguza uhaba wa madawati na viti, ikiwemo katika shule shikizi, huku ikitenga asilimia 10 ya mapato ya ndani kila mwaka kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya elimu.
“Hatutarajii kuendelea kuwa na uhaba wa madawati katika shule zetu shikizi kadri idadi ya wanafunzi inavyoongezeka, sambamba na uwepo wa walimu wa kutosha,” amesema Mweli.
Mkazi wa Igawa, Fatuma Juma, amesema uwepo wa shule shikizi umesaidia kwa kiasi kikubwa watoto wanaotoka maeneo ya pembezoni, hususan katika jamii zenye wafugaji wengi, kwa kuwa umepunguza umbali wa kutembea kwenda shule.
Naye Diwani wa Kata ya Rujewa, Makao Jeremiah, amesema kutambuliwa na kusajiliwa rasmi kwa shule shikizi kutakuwa jambo jema litakaloongeza motisha kwa walimu wanaofundisha katika shule hizo na kuboresha utoaji wa elimu.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi