November 24, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DED Lushoto aomba ushirikiano kwa madiwani kukamilisha miradi

lNa Yusuph Mussa, Timesmajira Online,Lushoto

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto mkoani Tanga Ikupa Mwasyoge amewaomba madiwani kutoa ushirikiano kwa viongozi wa Kata na Vijiji ili kuhakikisha miradi ya maendeleo ya wananchi haifanyiwi hujuma.

Amesema Diwani ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC), anatakiwa kushirikiana na viongozi wa kata na vijiji ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati huku ikiwa na ubora.

Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto wakiwa kwenye kikao cha mwaka cha Baraza la Madiwani Septemba 11, 2023.

Hayo ameyasema Septemba 11, 2023 kwenye kikao cha mwaka cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo na kueleza kuwa Serikali imeagiza kuwa hadi Septemba 30, mwaka huu miradi ya elimu iwe imekamilika huku miradi ya afya iwe imekamilika ifikapo Oktoba 31, mwaka huu.

“Madiwani, naomba tushirikiane kukamilisha miradi iliyopo kwenye kata zetu,tusisubiri mabaya yatokee, ndipo muanze kueleza bali mnapaswa kusimamia na kuona miradi hiyo inakamilika kwa wakati na viwango vinavyoku,mnatakiwa kushirikiana na viongozi wa vijiji ili kuweza kudhibiti mapema hujuma zozote zinazoweza kufanywa ili mradi ushindwe kukamilika, lakini kama mtasimama kwenye nafasi zenu, nina hakika miradi yetu itatekelezwa kwa ufanisi,”amesema Mwasyoge.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mathew Mbaruku (wa pili kushoto), Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Ikupa Mwasyoge (wa pili kulia) na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Hatibu Ulanga (kushoto), wakiwa kwenye kikao cha mwaka cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri hiyo Septemba 11, 2023.

Mwasyoge amesema moja ya kazi inayofanywa na halmashauri ni kuongeza mapato ya ndani ili kufanikisha hilo ni muhimu madiwani wakashirikiana na watendaji wa kata na vijiji ili wananchi waweze kuona umuhimu wa kulipa ushuru na tozo mbalimbali kwa ajili ya maendeleo ya halmashauri yao na taifa lao.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mathew Mbaruku amewatahadharisha baadhi ya madiwani kuacha kupiga simu ngazi za juu, pindi wanapoona miradi haiendi sawa kwenye kata zao badala yake wapige simu kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo, Mwasyoge, ili kumaliza changamoto hizo.

“Madiwani hawapaswi kupiga simu ngazi za juu au wizarani ili kuweza kutatua changamoto zilizopo kwenye kata zao bali wanatakiwa wampigie Mkurugenzi na kumueleza changamoto hizo,mnapopiga simu wizarani wao wanatupigia sisi, na kusema tumepigiwa simu na baadhi ya madiwani wenu,”ameeleza Mbaruku na kuongeza kuwa

“Labda niulize kama kuna diwani hapa amewahi kumpigia simu Mkurugenzi kwa ajili ya kumueleza shida zilizopo kwenye kata yake halafu asimsikilize, nyoosha mkono kama upo,hivyo tuache kupiga simu juu badala yake tutoe ushirikiano kwa Mkurugenzi ili tuweze kumaliza changamoto zetu,”.

Awali, Mkuu wa Wilaya ya Lushoto Kalisti Lazaro amesema madiwani ni wahanga wa miradi isiyokamilka kwani wataulizwa na wananchi kuanzia kwenye Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwakani na Uchaguzi Mkuu 2025, hivyo ili kukisaidia Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho sera zake ndiyo zinatekelezwa, basi waweze kusimamia miradi na ikamilike kwa wakati.

“Tunataka miradi yote ya viporo iishe na ikamilike ninyi madiwani ni wahanga wa Uchaguzi Mkuu 2025 pia ni kipimo kwenu kwa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa mwaka kesho kwa wenyeviti wenu wa vijiji na vitongoji,Diwani unatakiwa utoe mrejesho wa kile ulichofanya kwa mwaka 2020-2025, na sio kuanza kueleza utakachofanya (2025-2030)” amesema Lazaro.

Wakuu wa Idara na Vitengo wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto pamoja na viongozi wa vyama vya upinzani wakiwa kwenye kikao cha mwaka cha Baraza Septemba 11, 2023.

Kwenye kikao hicho, Diwani wa Kata ya Mbaramo Hatibu Ulanga alichaguliwa kwa mara ya tatu kuwa Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto.