January 12, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DED Ilemela akanusha wajawazito kujifungulia chini

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online Mwanza

Kufuatia picha iliyosambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha wajawazito wakipeana zamu kujifungua kwenye sakafu huku ikidaiwa ni katika kituo cha Afya Buzuruga Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela Wakili Kiomoni Kibamba amefafanua kuhusu tuhuma hizo.

Katika taarifa yake kwa umma iliotolewa Desemba 18,2023 Kimbamba ameeleza kuwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imeona taarifa ya picha ikisambaa katika mitandao ya kijamii ikionesha kuwa katika kituo cha Afya cha Buzuruga wakinamama wamekuwa wakipeana zamu kujifungua sakafuni.

Aidha ameeleza kuwa taarifa hiyo iliyosambaa kwenye mitandao ya kijamii imeenda mbali zaidi ikifafanua kuwa picha iliyotumika katika taarifa hiyo ni ya Septemba 2022.

Hata hivyo katika taarifa ya Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela imefafanua kuwa awali katika kituo hicho cha afya cha Buzuruga kulikuwa na vitanda vitatu kwa ajili ya kujifungulia, baada ya kuona kumekuwa na ongezeko la wakinamama wanaojifungua Serikali iliongeza idadi ya vitanda vya kujifungulia kutoka vitanda vitatu hadi vitanda sita.

Sambamba na hilo Serikali imejenga jengo la mama na mtoto lenye uwezo wa kulaza wakinamama 42, jengo hilo liligharimu kiasi cha milioni 200 fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri.

Lengo ikiwa ni kuondoa adha ya wakinamama kulala zaidi ya mmoja katika kitanda kimoja na jengo hilo lilizinduliwa na Mwenge wa Uhuru mwaka 2023 ambalo kwa sasa linatumika.

Hivyo kwa maelezo hayo,Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela, inapenda kuuhakikishia umma kuwa katika kituo cha afya cha Buzuruga, hakuna wakina mama wanaojifungulia chini kama taarifa ya mtandaoni inavyoonyesha.