Na Mwandishi wetu, TimesMajira Online
KLABU ya waandishi wa Habari Mkoa wa Dar es Salaam (DCPC) kwa kushirikiana na Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) kimelaani vikali kitendo kilichofanywa na Mkurungezi wa Manispaa ya Temeke, Lusubilo Mwakabibi dhidi ya Mwandishi wa Habari wa kituo cha ITV Richard Steven kwani ni udhalilishaji mkubwa kwa tasnia ya habari kwa ujumla na kumtaka kumuomba radhi Mwandishi huyo na tasnia ya habari kwa ujumla.
Akitoa tamko dhidi ya kitendo hicho, Mwenyekiti DCPC, Irene Meero amesema, kitendo kilichofanywa na Mkurungezi huyo ni udhalilishaji mkubwa si tu kwa Mwandishi huyo peke yake bali kwa tasnia nzima ya habari Nchini lakini ni wazi kuwa athamini haki ya waandishi kupata habari katika Manispaa yake na hatambui wajibu na haki za tasnia ya habari katika kuwajengea imani na serikali yao .
Amesema, mapema wiki hii mwandishi wa habari wa ITV alimpigia simu Mkurungezi wa Temeke Lusubilo Mwakabibi kuomba kwenda ofisini kwake kupata ufafanuzi wa suala la kuwepo kwa hali ya sitofahamu kati ya wananchi wa mtaa wa magogoni, Yombo Dovya baada ya Manispaa hiyo kuanza ujenzi wa Shule ya Sekondari Lumo.
Kutokana na sitofahamu hiyo wananchi walijitokeza kuzuia ujenzi huo kwa madai eneo hilo lina mgogoro ambao bado upo mahakamani .
Baadhi ya vyombo vya habari vilivyokuwepo katika eneo la tukio viliwahoji maofisa wa Serikali waliokuwepo ambao walisema mtu pekee mwenyewe Mamlaka ya kuzungumza kadhia hiyo ni Mkurungezi wa Manispaa hiyo, ndipo Mwandishi huyo wa ITV alipompigia Mkurungezi huyo na ndipo Mwandishi huyo aliamua kuomba kwa njia ya simu kwenda ofisini kwake kwa ajili ya kupata ufafanuzi.
Hata hivyo baada ya kupiga simu Mkurungezi huyo alipokea na kuanza kutoa kauli za kejeli na dhiaka “Wewe ni nani unaweza kupiga simu? Unasema unataka kuja kuniona? wewe ni Nani?.
Baada ya maswali hayo Mwandishi alirudia kujitambulisha pamoja na kumnyenyekea kwa kurudia kuomba kumuona, lakini Mkurungezi huyo aliendelea kutoa kauli iliyosheheni kiburi kwa kumtaka Mwandishi kujipima kama ana hadhi ya kukutana nae na kumtaka amwambie Mkurungezi wake (ITV) ndiye ampigie simu kwa vile yeye sio ‘level’ hadhi yake.
“Kitendo cha kukataa kutoa ushirikiako kwa wanahabari ni kuvunja sheria ya huduma za habari ya mwaka 2016 kifungu cha 7 kinachompa Mwandishi Mamlaka ya kukusanya na kuchakata na kuchapisha habari,” amesema Meero.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile amewataka viongozi kutambua umuhimu wa vyombo vya habari sambamba na kuwaheshimu waandishi wa habari.
Balile amesema, kutokana na sitofahamu hiyo iliyotokea baina ya waandishi wa habari na Mkurungezi huyo amewataka wanahabari kuendelea na majukumu yao ya kazi ikiwa ni pamoja na kwenda kuchukua habari katika Manispaa ya Temeke.
“Mkurungezi wa Manispaa ya Temeke anapaswa kutambua kuwa kazi hizi zinafanana hakuna kazi nzuri na iliyo bora kuliko yake na atufungia mtu kwani kufanya hivyo ni kuwanyima haki wananchi wa Manispaa ya Temeke,” amesema Balile.
More Stories
TAG yampongeza Rais Samia
CCM Tabora yamfariji mjane wa kada anayedaiwa kujiua
FDH yaanza kutekeleza mradi wa kuwajengea uwezo wanawake wenye ulemavu