Na Mwandishi Wetu. Mara
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) kwa kushirikiana na Vyombo vya Ulinzi na Usalama, ikiwemo Jeshi la Polisi, Jeshi la Akiba pamoja na wananchi imefanya operesheni kubwa ya kihistoria kwa muda wa wiki tatu katika wilaya ya Tarime na Serengeti, mkoani Mara kwa lengo la kukabiliana na tatizo la uzalishaji na usambazaji wa dawa za kulevya, hususani bangi.
Operesheni hiyo imefanyika katika vijiji vya Matongo, Nyarwana, na Weigita vilivyopo bonde la Masinki, pia vijiji vya Nkerege, Kembwe, Nyakunguru na Iseresere pamoja na eneo la bonde la mto Mara.
Akizungumza mara baada ya operesheni hiyo Oktoba 8, 2024, Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Aretas Lyimo amesema, jumla ya ekari 3,007.5 za mashamba ya bangi zimeteketezwa katika operesheni hiyo ambazo kilogramu 7,832.5 za bangi kavu, na kilogramu 452 za mbegu za bangi zilikamatwa, ambapo watuhumiwa 17 walikamatwa na tayari wamefikishwa mahakamani.
Kamishna Lyimo amesema, operesheni hiyo ni sehemu ya jitihada za Serikali kulinda jamii dhidi ya madhara ya dawa za kulevya na amesisitiza umuhimu wa ushirikiano kutoka kwa wananchi katika kutoa taarifa kuhusu shughuli zinazohusiana na dawa hizo.
Aidha Mamlaka imebaini kuwa, kilimo cha bangi mkoani Mara kinafadhiliwa na raia wa nchi jirani, ambao huwapa mitaji wakulima wa Tarime kisha bangi ikishakomaa huvunwa na kusafirishwa kwenda kuuzwa.
“Tunatoa miezi mitatu kwa wananchi wa mkoa wa Mara kuhakikisha wanaacha kabisa kujihusisha na kilimo cha bangi. Baada ya muda huo, tutafanya operesheni kubwa kwa namnna nyingine na kuhakikisha maeneo haya yanabadilishiwa matumizi na hayatumiki tena kwa kilimo cha bangi, Pia wote wanaotetea uhalifu huu watachukuliwa hatua ili kuhakikisha wanachi wote wanatii sheria za nchi”
Pia, Mkuu wa wilaya ya Tarim, Meja Edward Gowele amekiri wilaya yake kukabiliwa na changamoto ya kilimo cha bangi hususan katika eneo la bonde la mto Mara na tayari serikali imeanza kuchukua hatua madhubuti kukabiliana na changamoto hiyo.
“Tumeanza kutoa elimu kwa wananchi kuhusu madhara ya bangi na hasara wanayoweza kuipata kwa kujihusisha na kilimo cha bangi na walio wengi wametuahidi kuachana na kilimo cha bangi” amesema Gowele.
Kwa upande wake Mwita Mataro afisa wa maji kutoka bodi ya maji bonde la ziwa victoria dakio la Mara ambaye pia ni msimamizi wa rasilimali za maji katika mkoa wa Mara amesema, lengo kubwa la bodi ni kuhakikisha rasilimali za maji zinatunzwa na kuendelezwa pasipo kuruhusu uharibifu wa aina yoyote.
“Tumejionea hali halisi ya bonde na tumeshuhudia zao la bangi likiwa limelimwa katika bonde la mto Mara. Sheria za rasilimali za maji haziruhusu kilimo haramu cha zao la bangi. Hata mazao mengine halali yanapaswa kulimwa umbali wa mita 60 kutoka mtoni. Hao wanaolima bangi ni sehemu ya watu wanaoharibu vyanzo vya maji kwa sababu mwisho wa siku huu udongo wote mvua zitakaponyesha tope lote linatiririkka kwenda kwenye mto’’ amesema Mataro.
Ameongeza kuwa , Bodi hiyo imeandaa mpango kwa kidakio cha Kaskazini ambao unataja shughuli gani zinatakiwa kufanyika kwenye vyanzo vya maji ambazo ni rafiki, na wao kama bodi watasimamia kuhakikisha mipango hiyo inatekelezwa na hifadhi ya maji inalindwa.
Naye Lepapa Molel, ambaye ni Ofisa kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara amesema, wakulima wengi wanalima bangi kwa kutegemea maji yanayotoka mto Mara “Nashauri wakulima wageuke na kuanza kulima mazao ya chakula yanayoweza kuwapa chakula na fedha kuliko bangi”.
More Stories
SHUWASA yaboresha mtambo wa kuchakata takakinyesi
Daktari ajishindia milioni 100,fainali NMB Bonge la Mpango
Majaliwa ataka tenki la Kisesa lianze kutoa maji Februari