Na Mwandishi Wetu,Timesmajira Online
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini (DCEA) imewapiga msasa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari nchini kuhusiana na hatua inazochukua kupambana na dawa hizo, huku ikisema inathamini mchango mkubwa wa vyombo vya habari katika kuelimisha umma kuhusiana na dawa za kulevya nchini.
Hayo yamesemwa jana jijini Dar es Salaam na Kamishina wa Utawala na Huduma za Taasisi, Shaban Baraza wakati akizungumza kwa niaba ya Kamishna Jenerali wa Mamlaka ya Dawa za Kulevya (DCEA), Aretas Lyimo, kwenye ufunguzi wa semina ya siku mbili kwa wahariri wa vyombo vya habari nchini iliyoandaliwa na mamlaka hiyo.
“Waandishi ni wadau wetu muhimu sana katika mamlaka kwa sababu ninyi mpo katika jamii, pale mnapoona tatizo basi mnaweza kutupigia simu, kwamba kuna mahala kuna tatizo linaendelea.
“Kwa sababu tupo katika jamii huko, tunajua kinachoendelea, na siyo kwa wale wavutaji wadogo wadogo, lakini wale ambao mnadhani wapo katika mtandao wa dawa za kulevya.”
Kamishna Baraza alisema, jamii ikipata uelewa mpana kuhusu madhara ya dawa za kulevya itawasaidia kujiepusha na matumizi au biashara hiyo haramu nchini.
“Tangu mamlaka imeanzishwa vyombo vya habari vimekuwa na sisi katika kutoa taarifa kwa wakati,mmekuwa wepesi kujitokeza na kutupatia huduma.
“Wahariri ni watu muhimu sana katika kudhibiti dawa za kulevya, kwa sababu licha ya kuwa mhariri, pia wewe ni mzazi, lakini unaweza ukawa una ndugu zako.”
Alisema kuwa,kupitia mafunzo hayo, Mamlaka inaamini kuwa na wigo mpana wa kudadisi na kuhoji kuhusiana na masuala ya dawa za kulevya ili kuripoti taarifa sahihi kupitia vyombo vyao vya habari nchini.
Awali, Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kupitia DCEA, Florence Kambi alisema kuwa, lengo la semina hiyo ambayo ni mara ya pili kukutana na wahariri ni kuwajengea uelewa wa kutosha kuhusu dawa za kulevya.
“Katika kuhakikisha umma wa Tanzania unapata elimu kuhusu dawa za kulevya, katika kufanikisha hili mamlaka imeona ni muhimu kuvishirikisha vyombo vya habari habari hapa nchini.
“Kwani tunaamini kuwa ninyi ni wadau muhimu katika kuunganisha daraja la jamii katika kupata elimu kuhusu dawa za kulevya.
“Hivyo, ni vyema mkapata uelewa huu kuhusu dawa za kulevya ili kuweza kutoa elimu sahihi kwa jamii na taarifa kwa umma kama ilivyokusudiwa,”alisisitiza Kambi.
Pia, ameendelea kusisitia kuwa, lugha sahihi ya kuelezea kuhusiana na dawa za kulevya ni Dawa za Kulevya na wala si Madawa ya Kulevya.
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA) ilianzishwa chini ya kifungu cha 3 cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015. Sheria hii iliifuta Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya. Kuanzishwa kwa Mamlaka Kulitokana na mapungufu yaliyokuwepo katika mfumo wa udhibiti wa dawa za kulevya.
Mapungufu hayo yalikuwa ni pamoja na Tume ya Kuratibu Udhibiti wa Dawa za Kulevya iliyoanzishwa na Sheria ya ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995 kukosa nguvu ya kisheria ya kupeleleza, kufanya uchunguzi na kukamata wahalifu wa dawa za kulevya.
Kutokana na mapungufu hayo, Baraza la Mawaziri katika kikao chake cha tarehe 8 Novemba, 2007 (Waraka Na 60/2007) liliagiza, kurekebisha au kufuta Sheria ya Kuzuia Biashara Haramu ya Dawa za Kulevya Namba 9 ya mwaka 1995, ili kukidhi matakwa na changamoto za udhibiti wa matumizi na biashara ya dawa za kulevya.
Baraza la Mawaziri liliagiza kuundwa kwa chombo cha kupambana na dawa za kulevya chenye uwezo kiutendaji kwa kukipa mamlaka ya ukamataji, upekuzi na upelelezi kwa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ili kuongeza ufanisi wa udhibiti wa dawa za kulevya nchini.
Kufuatia agizo hilo, tarehe 24/03/2015 Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga na kupitisha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Na. 5 ya Mwaka 2015 na kuanza kutumika rasmi tarehe 15 Septemba, 2015 kupitia tangazo la Serikali namba 407 (GN NO.407/2015).
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ilianza kutekeleza majukumu yake kikamilifu tarehe 17 Februari, 2017 baada Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kumteua Kamishna Jenerali.
More Stories
CCM imejipanga kushinda kwa kishindo
Wanaotumia lugha za matusi,kashfa kwenye kampeni waonywa
Polisi Mbeya yawataka waandishi wa habari kutoa taarifa sahihi