May 8, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Majaliwa: WCF iko vizuri na utatunza familia yako

 

 Na Mwandishi Wetu, TimesMajira Online, LINDI

WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa amemuhakikishia Mnufaika wa Fidia inayotolewa na Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bi. Halima Sheikh Mbwana, kuwa ataendelea kuishi kwa furaha ikiwa ni pamoja na kutunza familia yake kwani WCF ipo.

Mhe. Majaliwa ameyasema hayo kwenye Mkutano wa 7 wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), mjini Lindi, Novemba 13, 2023, baada ya kusikiliza ushuhuda wa mnufaika huyo aliyepata ulemavu wa kudumu kufuatia kukatika mkono baada ya basi la abiria alilokuwa akiliendesha, Super Feo kupinduka Mei 22, 2022, wakati likiwa safarini kutoka Songea kueleeka Dar es Salaam.

“Mwenyezimungu ana matakwa yake na kila mmoja amempangia jambo lake na inshaallah, utaishi, utatunza familia yako kwani WCF wapo.” Alimuhakikishia Bi. Halima

Waziri Mkuu pia aliipongeza WCF kwa kumfuata Bi. Halima hospitalini baada ya kuarifiwa kuwa amepata ajali na kuumia.

“Nawashukuru sana WCF kwa kufanya na kutekeleza wajibu wenu, wa kumfuata mgonjwa hospitalini na kujitambulisha kwamba sisi ni ule Mfuko wa Fidia kwa Wanfanyakazi wanaoumia wakiwa kazini na kutambua kwamba dada yetu alikuwa kazini.”

Aidha Waziri Mkuu aliwahimiza waajiri kujisajili na Mfuko kwa manufaa yao na wafanyakazi wao, kwani ushuhuda uliotolewa na Bi, Halima mwenye watoto watatu ni ujumbe tosha kwa wao kufanya hivyo.

“Na ametoa ujumbe hapa kwa waajiri wote, jiungeni na WCF kwa usalama wa Wafanyakazi wenu wanapoumia wakiwa kazini wanalipwa fidia, na leo dada yetu anapata Mafao yake kila mwezi na yanamsaidia kuendesha maisha yake.” Alisisitiza Mhe. Majaliwa.

Awali wakati akitoa ushuhuda, Bi. Halima aliishukuru Serikali kwa kuanzisha Mfuko huo ambao umeweza kumfariji baada ya kukumbwa na changamoto hiyo.

“Nilipopata ajali na kupelekwa hospitali, watu wa WCF walinitembelea na kunieleza jinsi Mfuko utakavyonihudumia, na kweli wamenihudumia matibabu hadi kupona na kunipatia mkono wa bandia.” Alisema.

Alisema, licha ya huduma hizo, bado WCF inamlipa mafao kila mwezi yanayomuwezesha kuendesha maisha yake na familia yake.

“Sikuwahi kuwaza kama nitakuja kuwa na faraja, nilikuwa na asilimia 90 ya furaha na WCF wamejazia asilimia 10, na kuniweka vizuri na kunionyesha upendo, hivi sasa nikitembea huwezi kujua kama nina kiungo bandia, ninatembea, ninadunda kwa furaha.” Alisema.



WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, akizungumza kwenye mkutano wa 7 wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Mkoani Lindi Novemba 13, 2023
WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, akizungumza kwenye mkutano wa 7 wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Mkoani Lindi Novemba 13, 2023

Bi. Halima Sheikh, akitoa ushuhuda mbele ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa ambaye alikuwa mgeni rasmi kwenye mkutano wa 7 wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Mkoani Lindi.
Meza Kuu.
WAZIRI Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, akizungumza kwenye mkutano wa 7 wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Mkoani Lindi Novemba 13, 2023

Baadhi ya Wahariri wa vyombo vya habari waliohudhuria mkutano huo