November 6, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DCEA yakoleza kasi kuteketeza mashamba ya bangi nchini

Na David John timesmajira Online

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Nchini (DCEA) kwa kushirikiana na vyombo vingine vya Ulinzi na Usalama wakiwemo JKT Ruvu imefanya operesheni ya siku nane mfululizo mkoani Morogoro na kufanikiwa kukamata jumla ya gunia 131 za bangi kavu,kilo 120 za mbegu za bangi, watuhumiwa 18 pamoja na kuteketeza hekari 489 za mashamba la mmea huo.

Askari wa JKT wakiwa katika operesheni ya kuharibu bangi katika Wilaya za Mvomero ,Morogoro Vijijini ikiwa ni mwendelezo wa kidhibiti na kupambana na dawa la kulevya nchini

Ambapo operesheni hiyo imefanyika katika Wilaya za Morogoro, Morogoro vijijini na Mvomero hivyo kwa Wilaya ya Morogoro Vijijini Kata ya Kisaki na kijiji cha Rumba zimekamatwa gunia 70 za bangi, Kijiji cha Mbakana zimekamatwa gunia 59 za bangi, kilo 120 za mbegu za bangi na kuteketezwa hekari 350 za mashamba ya bangi.

Kwa mujibu ya taarifa hiyo iliyotolewa leo Agosti 2 mwaka huu na Kamishna Jenerali wa Kudhibiti na kupambana na dawa za kulevya nchini Aretas Lyimo imesema wilayani Mvomero mamlaka imeteketeza hekari 139 na Wilaya ya Morogoro zimekamatwa gunia mbili (2) za bangi.

Akizungumza zaidi wakati wa operesheni hiyo, Kamishna Jenerali Lyimo amesema wakulima wa bangi mkoani Morogoro wanalima pembezoni mwa mto na kukata miti ili wawezekupata maeneo ya kulima bangi.

“Wakulima wa bangi wa Mkoa huu wanachepusha maji na kuyazuia yasiende kwenye maeneo mengine yakahudumie wananchi kwa lengo la kumwagilia mashamba yao, wanafanya uharibifu mkubwa wa mazingira kwa kukata miti katikati ya msitu ili waweze kulima bangi hivyo kusababisha uharibifu mkubwa wa mazingira ikiwemo kuharibu vyanzo vya maji katika maeneo haya,” amesema kamishna Jenerali Lyimo.

Amesema kwamba, wakulima wa bangi wanalima mashamba yao katika maeneo ya mbali yaliyojificha na yasiyoweza kufikika kirahisi lakini mamlaka hiyo ya imeweza kuyafikia maeneo hayo na kuwakamata wanaojihusisha na bangi pamoja na kuteketeza bangi iliyovunwa pamoja na mashamba.

“Kwa mfano katika maeneo haya ya Morogoro ambayo tumefanya hii operesheni eneo ambalo wamelima bangi ni mbali kutoka mjini,kutoka unapoliacha gari mpaka kufika huku unatembea masaa sita mwendo wa kijeshi,kwaio wanaamini hakuna mtu anayeweza kufika,” amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Hata hivyo amewaasa waanchi kutoa taarifa juu ya watu wanaolima bangi na mirungi ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.

“Wananchi wote Tanzania watusaidie kutoa taarifa za wakulima wa bangi na mirungi katika maeneo mbalimbali ili tuwakamate na kuharibu mashamba yao,kwani mbali na madhara mengine yanayotokana na zao la bangi, wakulima hawa wanaharibu misitu, vyanzo vya maji, na wanaweza kutengeneza jangwa, “amesema.

Amesema wakulima hao wanalazimika kukata miti sana ili wapate maeneo ya kulima bangi lakini Kulingana na taarifa ya hali ya dawa za kulevya ya Mwaka 2022, Mkoa wa Morogoro ni kati ya mikoa mitano iliyokithiri kwa kilimo cha bangi nchini.