*Watuhumiwa saba wahusishwa kuingiza nchini kama mbolea
*Kamishna Jenerali Lyimo atoa onyo
Na Agnes Alcardo, Timesmajira
MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA),imekamata shehena ya dawa mpya za kulevya aina ya mitragyna speciosa mifuko 756 yenye uzito wa kilogramu 18,485.6 sawa na tani 18.5 iliyokuwa ikiingizwa nchini kama mbolea.
Hayo yamesemwa Agosti 13,2025 na Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam.

Jenerali Lyimo,amesema katika tukio hilo watuhumiwa saba wamekamatwa, wakiwemo raia wawili wa nchi ya Sri – Lanka ambao ni Jagath Prasanna Madduma Wellalage (46) na Santhush Ruminda Hewage (25).
Amesema,Watanzania waliokamatwa ni Riziki Shawej(40), Andrew Nyembe (34), Mariam Mgatila (40), Ramadhan Said (57) na Godwin Maffikiri (40).
“Dawa hizi zilikuwa kwenye kontena lenye ukubwa wa futi 40, zikitokea nchini Sri -lanka,hii ni mara ya pili kukamatwa kwa aina hii ya dawa mpya za kulevya.Juni mwaka huu, tulikamata mifuko 450 yenye zaidi ya uzito wa tani 11.5 za dawa hizo aina ya mitragyna speciosa iliyoingizwa nchini kama mbolea ikiwa kwenye kontena lenye ukubwa wa futi 20 ikitokea nchini Sri – Lanka ikiwahusisha watajwa hapo juu,”amesema Jenerali Lyimo na kuongeza:
“Hivyo, kufanya jumla ya kilogramu 30,082.03 sawa na tani 30 za dawa hizo kukamatwa kwa kipindi kifupi hapa nchini,”.
Kamishna Jenerali Lyimo amesema kuwa, Mitragyna Speciosa ni dawa mpya ya kulevya (New psychtropic Substance-NPS) inayotokana na mmea unaofahamika kwa jina la Kratom ambao hupatikana zaidi katika nchi za Kusini Mashariki mwa Bara la Asia.Pia ina madhara sawa na dawa za kulevya jamii ya Afyuni (Heroin, Morphine).
“Dawa hii huathiri mfumo wa fahamu pamoja na kusababisha uraibu na vifo vya ghafla. Kutokana na kuongezeka matumizi ya dawa ya Mitragym Speciosa duniani, pamoja na madhara yanayosababishwa na sumu zilizomo katika dawa hii, nchi nyingi duniani zimezuia uzalishaji, usafirishaji na matumizi yake,”.
Hata hivyo amesema,ukamataji wa Mitragyna Speciosa ni ishara ya kuwepo kwa changamoto mpya katika vita dhidi ya dawa za kulevya nchini.Hivyo wataendelea kuimarisha ufuatiliaji na udhibiti zaidi wa biashara ya dawa hiyo pamoja na dawa nyingine za kulevya hapa nchini.

.
Amesisitiza kuwa matumizi na biashara ya dawa za kulevya yana madhara mbalimbali yakiwemo ya kiafya, kijamii na kiuchumi,hivyo,vita dhidi ya dawa za kulevya kutabadilisha mtindo wa maisha unaozingatia misingi iliyowekwa na kufikia malengo ya Dira ya Taifa mwaka 2050 kwa ufanisi, kwa kuhakikisha dawa za kulevya zinatokomezwa nchini na kulinda nguvu kazi ya taifa.
“Tunaendelea na kasi ya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini, ikiwemo kuvunja mitandao ya dawa za kulevya na kubaini mbinu mpya za biashara na matumizi ya dawa hizo,kuongeza wigo wa utoaji elimu juu ya madhara ya dawa za kulevya kwa lengo la kujenga jamii imara na kulinda ustawi wa jamii kwa maendeleo endelevu,”amesisitiza Kamishna Jenerali Lyimo.


More Stories
TAMWA yakumbusha jamii kupinga ukatili wa kijinsia kuelekea siku ta wanawake Duniani
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro