January 23, 2025

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC wa Nyang’hwale afariki

Na Penina Malundo

MKUU wa Wilaya ya Nyang’hwale mkoani Geita, Hamim Buzohera Gwiyama, jana saa 5:00 asubuhi katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando baada ya kuugua kwa muda mfupi.

Taarifa iliyotolewa leo kwa vyombo vya habari Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais — TAMISEMI, Seleman Jafo, kusainiwa na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Rebecca Kwandu, imeeleza kuwa Serikali inatambua na itaendelea kuenzi mchango wa Marehemu katika ujenzi wa Taifa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Marehemu Gwiyama aliteuliwa na Rais John Magufuli kushika nafasi ya Mkuu wa Wilaya ya Nyang’hwale Juni 26, 2016 ambapo kabla ya uteuzi huo aliwahi kufanya kazi sehemu mbalimbali nchini.

“Serikali inatambua na itaendelea kuenzi mchango wa Marehemu Hamim Buzohera Gwiyama katika ujenzi wa Taifa hili,”ilieleza taarifa hiyo.

Waziri Jafo alitoa salamu za pole kwa Mkuu wa Mkoa wa Geita, Robert Gabriel, Mkuu wa Mkoa wa Geita, wananchi wa wilaya ya Nyang’hwale, familia ya marehemu, ndugu na jamaa wote walioguswa msiba huu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa taratibu zingine za mazishi zitaendelea kutolewa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Geita.